WAZIRI MKENDA AZINDUA MFUMO WA KIZIMBA KUVUTIA VIJANA KATIKA KILIMO .

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA KILIMO

Anuani yaSimu: “Kilimo Dodoma                        Idara ya Utawala,

Nambari: +255 26 2321407                                  Mji wa Serikali Mtumba,

Fax:  +255 26 2320037                                        S.L.P.  2182,

Email: ps@kilimo.go.tz                                    DODOMA.

 

 

TAARIFA KWA UMMA: WAZIRI MKENDA AZINDUA MFUMO WA  KIZIMBA KUVUTIA VIJANA KATIKA KILIMO

 

Morogoro 16.03.2021

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amezitaka taasisi za fedha nchini kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuwavutia vijana wengi kujikita katika kilimobiashara kupitia mfumo wa Kizimba ‘Business Model’ unaoratibiwa na Taasisi ya SUGECO.

Akizundua mfumo huo  mjini Morogoro leo (16.03.2021) Prof. Mkenda mbali ya kuupongeza,amesema  mfumo wa Kizimba utawezesha vijana wengi kujiunga pamoja kama ushirika na kutumia ardhi kuanzisha shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo kwa usimamizi wa wataalam wa taasisi hiyo.

“Wito wa serikali kwa taasisi za kifedha hapa nchini nikutoa mikopo yenye riba nafuu ili waweze kuanzisha shughuli za kilimo kupitia mfumo huu wa kizimba ambapo utasaidia  kuongeza tija na uzalishaji mazao ya kilimo hali itakayochochea ukuaji wa ajira na kuongeza kipato kwa vijana ” alisema Waziri Mkenda.

Ili kukuza tija na uzalishaji kwenye sekta ya kilimo Prof. Mkenda amesema wizara yake itaendelea kuhamasisha kujengwa kwa miundombinu ya umwagiliaji pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo bora na huduma za ugani hatua itakayokuza tija kwenye kilimo.

Aliongeza kusema kuwa taasisi ya SUGECO inayoundwa na wahitimu inafanya kazi nzuri ya kuwaunganisha vijana wanaofanya kazi za kilimo kwa kuwapatia mafunzo kwa vitendo na kuwaunganisha na masoko.

“Sekta ya kilimo kinachangia chini ya theluthi moja kwenye pato la taifa (28%)  na kwa upande wa kilimo mazao  bado mchango wake ni chini na takribani theluthi mbili ya nguvu kazi ya watanzania inajishughulisha na kilimo hivyo tafsiri yake ni kuwa tija yetu bado ipo chini..Tunataka tuongeze tija ili kilimo kichangie zaidi kwenye ukuaji wa uchumi” alisisitiza Prof.Mkenda

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Sokoine Prof.Raphael Chibunda alisema chuo hicho kitaendelea kushirikiana na wizara ya kilimo kusukuma na kubadilisha mfumo wa kilimo kuwa wa kibiashara ambapo sasa kiefanikiwa kuanzisha mashamba biashara kwenye maeneo yote ya chuo.

Prof. Chibunda aliongeza kusema taasisi ya SUGECO inafanya kazi zake kwa kutoa mafunzo ya vitendo kupitia vitalu nyumba zaidi ya 100 kufundisha vijana stadi za kilimo biashara hatua inayochangia kukuza ajira na kipato kwa vijana.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SUGECO Revocatus Kimario alisema mfumo wa kizimba Bussines Model ulizindiliwa utawezesha vijana wengi kukutana na wadau wa kilimo ikiwemo taasisi za fedha kwa ajili ya mitaji na wataalam wa ugani hatua itakayokuza uzalishaji wa mazao .

Kimario alisema Kizimba Bussiness Model unalenga kubadili fikra na mitizamo ya vijana kuhusu kilimo  ambapo itafanya waone kilimo ni ajira kama zilizvyo ajira zingine kupitia vikundi kwenye halmashauri ambapo kilimo vizimba itaanzishwa.

“Mfumo wa kizimba utapunguza vihatarishi kwa wakulima kwani watapata huduma kwenye eneo moja chini ya uratibu wa wataalam na uwepo wa uhakika wa soko ambapo tatizo la ajira litapungua kwa kiasi kikubwa” alisema Kimario.

Mwisho

Imetolewa na;

 Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

MOROGORO

 

 

Post a Comment

0 Comments