DKT SERERA AKIRI MCHANGO WA WANAHABARI,CPC 'YAMWAGA' TUZO KWA WADAU

 


📌HAMIDA RAMADHANI

MKUU wa Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma Dkt.Seleman Serera  amesema  tasnia ya Habari ina mchango mkubwa katika kuibua changamoto za jamii ili kuweza kutatuliwa na serikali.

Mkuu huyo wa wilaya amebainisha hayo leo leo 8,2021  katika maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya Habari mkoa wa Dodoma yaliyoandaliwa na Klabu ya  Waandishi wa Habari mkoa wa Dodoma (CPC) kwa kushirikiana na Umoja wa  Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC),Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA)pamoja na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira jijini Dodoma (DUWASA).

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge ,mkuu huyo wa wilaya amesema vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi  huku pia akiwataka wanahabari kuendelea kuwa na ubunifu katika uchakataji wa habari .

Vyombo vya habari vinatoa hamasa kubwa katika maendeleo ya nchi.Waandishi mmeibua changamoto nyingi ambazo nyingine sisi viongozi hatuwezi kuziona.Lakini mnavyozionesha mnatupa fursa sisi kuzitatua na kuboresha maisha ya wananchi.

Dkt.Seleman Serera 

Katika hatua nyingine  amewataka wanahabari kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na kuhakikisha wanaandika habari zenye mizania (balance) ili kuweza kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.

Mwenyekiti wa CPC Musa Yusuph akitoa neno

Mwenyekiti wa klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa  Dodoma (CPC) Musa Yusuph ameainisha changamoto zilizopo katika tasnia ya   habari ikiwemo mialiko isiyozingatia uzito wa matukio ya kihabari.

Mwenyekiti huyo amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wadau wa habari ambao wamekuwa wakitoa mialiko kwa vyombo vichache vya habari huku wakijua jambo hilo ni nyeti na linahitajika kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Tuwaombe wenzetu mnaoratibu matukio au habari za viongozi wa Umma,habari hizo kila mwandishi anazihitaji hivyo unapoalika vyombo vichache ni kuwanyima Watanzania haki yao kupashwa habari.

Mussa Yusuph

Naye Katibu Mkuu wa Klabu hiyo Ben Bago amewasihi baadhi ya Wadau wa Habari kuacha tabia ya  kutoa lugha isiyokuwa na staha kwa wanahabari pindi wanapotekeleza majukumu yao.

Katibu huyo amebainisha kwamba baadhi ya wadau wamekuwa kwenye migongano ya mara kwa mara na waandishi kutoka na kauli za kejeli na dharau zinazotolewa.

Malalamiko mengi tunayopokea ni kuhusu baadhi ya wadau kuwatolea lugha zisizo na staha kwa waandishi,tujifunze kuvumiliana na tutambue wote lengo letu ni kufikisha taaluma kwa umma

Ben Bago

Afisa Mhifadhi mkuu Mamlaka ya Hifadhi Tanzania
 (TANAPA) Jully Lyimo akitoa mada

Afisa Mhifadhi mkuu Mamlaka ya Hifadhi Tanzania (TANAPA) Jully Lyimo pamoja afisa utalii mkoa wa Manyara Cecilia Nkwabi wamelezea mchango wa Habari katika sekta ya utalii nchini ambapo wamesema  waandishi wa habari na Sekta ya utalii ni kama mapacha hivyo wanasaidiana katika kazi.

Pia TANAPA imetoa Wito kwa Watanzania kutembelea hifadhi za taifa ili kujifunza mambo mbalimbali huku wakibainisha kuwa mamlaka hiyo ipo mbioni kuanzisha Utalii wa Michezo (sports Tourism).

Sanjari na hilo CPC imetoa tuzo kwa wadau mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa watu na taasisi ambazo zinachangia ustawi wa tasnia ya habari katika mkoa wa Dodoma.



Mgeni rasmi Dkt.Seleman Serera (katikati) akimkabidhi tuzo Afisa Mhifadhi mkuu
Mamlaka ya Hifadhi Tanzania (TANAPA) Jully Lyimo


Mgeni rasmi Dkt.Seleman Serera (katikati) akimkabidhi tuzo Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya
Maji na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA) Bw.Sebastian Warioba 

Tuzo hizi ni endelevu,tunahitaji kuona ushirikiano kati ya Waandishi na Wadau wa Habari unaimarika,hivyo kila mwaka tutatoa tuzo ili kuwatambua wale wanaowezesha wanahabari kufanya kazi katika mazingira rafiki. 

Ben Bago.

Katika tuzo TANAPA na DUWASA walipokea tuzo kwa upande wa taasisi zenye mchango mkubwa kwa waandishi wa habari,huku Afisa Uhusiano wa TANESCO mkoa wa Dodoma Innocent Lupenza akipokea tuzo ya Afisa Habari bora wa mwaka.

Lupenza ameibuka mshindi baada ya kuwashinda wapinzani wake wa karibu Catherine Sungura (Wizara ya Afya) na Everlyn Thomas (Ofisi ya CAG).

Mapendekezo ya majina na kura hizo zilipigwa na Wanachama wa CPC ilikumpata mshindi ambaye vigezo vikuu ni ushirikiano (kufikika,kauli nzuri na Msaada kwa waandishi) kwa Waandishi wakati wanatimiza majukumu yao.

Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na washindi wa tuzo

Pia Sebastian Warioba amepata tuzo ya mwanachama bora wa CPC kwa mwaka 2020-2021.Warioba ametunukiwa tuzo hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya klabu hiyo ya makao makuu ya nchi.

Maadhimisho ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani kitaifa yalifanyika Mei 3, 2021  Jijini Arusha ambapo mkoa wa Dodoma yamefanyika Mei,8,2021 yakienda sambamba na kaulimbiu isemayo Habari kwa Manufaa ya Umma .

Post a Comment

0 Comments