JAFO ATAKA JAMII NA WADAU KUTUNZA MAZINGIRA KWA UCHUMI ENDELEVU

 



 ðŸ“Œ PENDO MANGALA

 

WAZIRI wa Muungano na Mazingira Seleman Jafo ameitaka jamii pamoja na Wadau mbalimbali kuhakikisha wanazingatia suala zima la utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi kwani nchi haiwezi kupata uchumi endelevu endapo itashindwa kutunza mazingira.

 

Waziri Jafo ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayojihusisha na masuala ya mazingira kwa lengo la kufahamiana pamoja na kutengeneza mtandao wa utendaji kazi.

 

 “ lengo la Serikali ni kuhamasisha utendaji kazi wa Asasi hizo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu stahiki na kuimarisha uratibu wa shughuli za Usimamizi wa Mazingira nchini na kudumisha mahusiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Asasi zisizo za Kiserikali zinazohusu Hifadhi ya Mazingira;”Alisema

 

Aidha amesema kama Serikali wamekuwa na afua mbalimbali licha ya bajeti ya mazingira kuwa ndogo lakini watahakikisha suala la mazingira wanalipa kipaumbele huku akiwataka wadau hao   kujikita zaidi katika usimamazi wa mazingira kwa kushirikiana na Serikali ili kuratibu shughuli za Mazingira kwa ufanisi zaidi katika Mikoa yote..

 

“Nafahamu, nyinyi mmekuwa wadau wakubwa katika hifadhi ya mazingira nchini na mmekuwa mkijitoa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu agenda hii muhimu ya mazingira kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo,” Waziri Jafo alisisitiza.

Hata hivyo Waziri Jafo amezitaka asasi hizo kusogeza huduma katika maeneo mengi nchini ili kuleta tija na kupambana na uharibifu wa mazingira ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na shughuli za kibanadamu zisizo endelevu.

“Ndugu zangu hatuwezi kupata uchumi endelevubila kudhibiti mazingira yetu, uharibifu wa mazingira duniani ni wakutisha, athari za mabadiliko ya tabianchi nsi kubwa na kumekuwa na ongezeko la kina cha maji katika Mito, Mabwawa na Maziwa kutokana kuongezeka kwa mvua juu ya wastani,” Jafo alisisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira kutoka  Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,Dk Andrew Komba amesema kuwa Serikali imekuwa na miongozo mbalimbali ya mazingira ikiwemo Sera ya Mazingira pamoja na mpango wa maendeleo huku akisema  vipaumbele vya Serikali ni kumaliza changamoto za utendaji kazi na  Asasi za kiraia.

 Amesema kuwa kikao hicho kimefungua sura mpya  baina ya Asasi hizo za kiraia na Serikali kwani hapo awali zimekuwa zikitekeleza mipango yake bila kuzingatia vipaumbele vya Serikali.

Naye Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo Bi. Winifrida Shonde kutoka Asasi ya Tanzania Environment and Empowerment Movement (TEEM) aliishauri Serikali kuhakikisha kila Asasi  ya kiraia kupewa majukumu ya kuainisha malengo katika hifadhi ya mazingira.

 

“Naamini Serikali kwakufanya hivi itasaidia kuweka utaratibu bayana wa utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa mazingira hapa nchini,”alisema

 

Katika kikao hicho baina ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGOs, CSOs & CBOs) kimehusisha takribani washiriki Mia Mbili kote nchini.

Post a Comment

0 Comments