TANZANIA YAJIPANGA KUIPAISHA PARETO AFRIKA




 MWANDISHI WETU

TANZANIA imedhamiria kuendelea kuongoza barani Afrika kwa uzalishaji wa zao la pareto toka tani 3000 mwaka 2021 hadi kufikia malengo ya tani 9,000 kutokana na uwepo wa viwanda vitatu vya kuongeza thamani zao hilo.

Hayo yamebainishwa leo (28.05.2021)  jijini Dodoma wakati wa kikao cha wadau wa zao la pareto toka mikoa sita nchini kilichoshirikisha viongozi wa mikoa, wilaya ,halmashauri, makampuni ya pareto na wawakilishi wa wakulima.

Akizungumza kwenye kikao hicho Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliwapongeza wadau kwa kuweka lengo hilo la kufikisha tani 9,000 za maua ya pareto ambapo viwanda vitatu vilivyopo sasa vitaweza kuinunua yote kulingana na uwezo wake.

Bashe alisema ili kufikia malengo hayo ya uzalishaji wizara kupitia Bodi ya Pareto na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) itawekeza kwenye utafiti wa mbegu bora za pareto na kuhakikisha zinapatikana kwa wingi na kugawiwa kwa wakulima nchini.

Tunahitaji mbegu bora za pareto tani 3 ili zitumike kuzalisha tani 9,000 za pareto baada ya mwaka mmoja  ambapo viwanda viko tayari kuinunua toka kwa wakulima

Bashe

Naibu Waziri huyo alizipongeza  Kampuni ya  Pareto Tanzania (PCT) ambayo itanunua tani 6,000 kwa mwaka huku kampuni ya TAN Extract Ltd ikihitaji tani 1,000 na kampuni ya PYTECH Ltd  ikihitaji tani 2,000 za maua ya pareto itakayozalishwa na wakulima msimu wa 2022/23.

Katika hatua nyingine Bashe alibainisha mikakati ya wizara kuhakikisha zao la pareto linakuwa na tija na uzalishaji wake unaongezeka zaidi ambapo alitaja mambo sita .



Kwanza kuongeza utafiti na uzalishaji wa mbegu bora tani 3 kupitia TARI,  pili kuanzisha mfumo wa kilimo mkataba (Contract Farming), tatu kuanzisha mfumo wa ushirika kwa kuanzisha AMCOS za wakulima wa pareto.

Mkakati wa nne ni kuhamsisha Halmashauri kutenga  mashamba vitalu (Block Farming )kisha kugawa kwa wakulima ambapo lengo kuanzia ekari 200 ,tano ni kusajili na kuwatambua wakulima wa pareto na sita wizara itaendelea na juhudi za kuondoa migogoro baina ya wanunuzi kwa kutenga kanda ( Zone of production).

Kwa upande wake  Mkulima bora wa zao la pareto Mzee Anangisye Mwankina kutoka Kata ya Ipelele Kijiji cha Makwaranga Tarafa ya Magoma wilaya  ya Makete ametoa ombi kwa wizara ya Kilimo kuwashirikisha  viongozi wa wilaya nchini kutoa ushirikiano wa karibu kwa wakulima wa pareto ili ubora wa zao uongezeke hatua itakokuza bei.

Mwankina ambaye amekuwa mkulima bora wa pareto tangu mwaka 2014 hadi sasa ametoa ombi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kutembelea wakulima wa Makete hatua itakayoongeza ari ya Kilimo hicho.

Ninalima ekari  3 ambapo kwa mwaka navuna kilo 800 na ubora wangu umefikia 1.8% lakini tatizo letu mabenki yanatukopesha kwa riba kubwa mno hatua inayotukwamisha. Tufikishie salamu kwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan aje  atutembelee Makete.

Mzee Mwankina.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Pareto nchini Lucas Ayo alisema uzalishaji wa zao la pareto umeongezeka toka tani 2,011 mwaka 2015/16 hadi kufikia tani 2,510 mwaka 2019/20 kati ya lengo la kuzalisha tani 3,000.

Aidha alibainisha kuwa tija imeongezeka toka wastani wa kilo 250 kwa ekari mwaka 2015/16 hadi kufikia kilo 270 kwa ekari mwaka 2019/20 huku wastani wa bei ya chini anayolipwa mkulima imepanda toka shilingi 1500 mwaka 2015/16 hadi shilingi 2,400 mwaka 2019/20 na shilingi 2,500 mwaka 2020/21 kwa kilo moja ya pareto.

Ayo alitaja mkakati wa Bodi ya Pareto katika mwaka 2021/22 ni kuongeza utafiti wa kina kuhusu matumizi mbalimbali ya bidhaa za pareto ikiwemo visumbufu vya mimea mashambani, majumbani na kwenye maghala ya mazao hatua itakayochochea kukuza kilimo na tija cha zao la pareto.

Naye   Mbunge wa Mbeya Vijijini  Oran Njeza alisema wakulima wa Mbeya vijijini wanaomba Wizara ifanye zao la pareto kuwa zao la kimkakati kwani ndilo linategemewa zaidi kimapato.

Mdau huyo alitoa wito kwa Wizara ya Kilimo  ichukue hatua za haraka kuisaidia bodi ya pareto kifedha na watumishi ili isimamaie zao hili kwa ufanisi na kuwa sasa bodi haifanyi vizuri kwenye usimamizi wa zao hatua inayopelekea wakulima wakate tama.

Zao la pareto kwa muda mrefu limekosa ushindani hatua inayosababisha liwe na bei ndogo, hivyo wizara ihamasishe wawekezaji zaidi wa viwanda vya kuongeza thamnai zao la pareto

Njeza.

Kuhusu suala la kutenga maeneo ya kilimo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga alisema wamelenga kuongeza eneo la uzalishaji pareto toka ekari 40 za sasa hadi kufikia ekari 100 kwa kutumia Block Farming hatua itakayokuza uzalishaji ambapo msimu huu wamezalisha tani 4.3 za pareto .

Zao la pareto kwa sasa linalimwa kwenye mikoa ya sita ya  Arusha, Manyara, Songwe, Njombe na Iringa ambapo Bodi  imefanikiwa hadi kufikia Februari 2021 imesajili  wakulima 10,586 kwenye mfumo wake wa utambuzi na huduma kwa wakulima.

                                      

Imeandaliwa na ;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

DODOMA

 

 

Post a Comment

0 Comments