UHAMIAJI YAWASIMAMISHA KAZI MAAFISA WALIOMRUSHA 'KICHURA' MTUHUMIWA



 ðŸ“ŒSALEH RAMADHANI

IDARA ya uhamiaji imewasimamisha kazi askari watatu wa jeshi hilo ili kupisha uchunguzi kwa tuhuma za kutumia nguvu  kinyume cha sheria na maadili ya kazi zao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini hapa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna Makakala amebainisha kuwa hatua hiyo imekuja kutokana na  video fupi iliyokuwa ikisambaa mtandaoni ikiwaonyesha askari hao  wakitumia nguvu kumkamata Alex Kyai  ambaye ni mtuhumiwa wa makosa ya kiuhamiaji.

Idara ya Uhamiaji inakiri kutokea kwa tukio hilo na pia inalaani kitendo kilichofanywa na askari hao kwa kutumia nguvu kinyume cha sheria na maadili ya kazi zao; hata hivyo idara ya uhamiaji tayari imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya askari hao ikiwemo kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yao

Kamishna Jenerali  huyo amebainisha kuwa tukio hilo lilitokea Mei 27 mwaka huu katika ofisi ya uhamiaji kurasini Jijini Dar es Salam ambapo mtuhumiwa huyo alifika ofisini hapo na mteja wa paspoti za uhamiaji ambaye alimtambulisha kama mke wake.

Dkt Makakala amesema baada ya mahojiano ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa na tabia ya kuwalaghai na kupokea fedha kutoka kwa wateja mbalimbali ili aweze kuwapatia  pasipoti haraka haraka. 

Hata hivyo tumebaini kuwa na matukio ya aina hiyo mengi ikiwemo  kujitambulisha kama mtumishi wa Taasisi nyeti ikiwemo ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili aweze kujipatia fedha kutokakwa watu mbalimbali wenye shida zinazofanana na taasisi hiyo

Hata hivyo Dkt.Makakala amesema Mtuhumiwa huyo  bado anaendelea kuhojiwa ili kujilisdhisha kuhusu tuhuma zake   kwani amekuwa na matukio ya kulaghai mengi na kwa muda mrefu.

Kamishna Jenerali Dk Anna amewataka wananchi wanaotaka huduma za uhamiaji kufika kwenye ofisi ili kuepusha utapeli ambao unaweza kujitokeza dhidi yao.

Alisisitiza kuwa idara ya uhamiaji itaendelea kutoa huduma zake kwa weredi,uwazi na bila kutumia mtu kati na kuwataka wananchi kutoa taarifa za watu wanaofanya vitendo vya kilaghai.

Natoa onyo kwa mtu yoyote ambaye atajaribu kujifanya kuwa yeye ni afisa Uhamiaji au afisa yoyote wa serikali ili kumsaidia mtu mwingine kwa maslahi yake binafsi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria.

Idara ya Uhamiaji inaendelea kuomba kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa kutoa Taarifa za watu wanaofanya vitendo vya aina hii.

 

Post a Comment

0 Comments