WATOA HUDUMA WATAKIWA KUJENGA TABIA YA KUHAKIKI VIPIMO VYA HUDUMA

 


📌PENDO MANGALA

WAKALA  wa Vipimo Mkoa wa Dodoma(WMA)  imewataka watoa huduma za afya Mkoani hapa kujenga tabia ya kuhakiki vipimo vya huduma ili kulinda afya za Wananchi huku ikiitaka jamii kwa ujumla kutumia mizani  iliyowekwa stika na nembo za wakala wa vipimo.

Kaimu Meneja wa Wakala wa vipimo Mkoa wa Dodoma  Karim Zuberi ameyasema hayo  wakati akizungumza na vyombo vya habari baada ya kutembelea vituo vinavyotoa huduma ya mizani ikiwemo Hospitali ya KCMC Pamoja na kituo cha kufanyia mazoezi cha Home fitness  ikiwa siku ya maadhimisho ya vipimo Duniani. 

Meneja huyo alisema lengo la siku ya vipimo duniani  ni kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi huku akitaja jukumu kuu la Wakala wa Vipimo kuwa ni kumlinda mlaji kupitia matumizi ya vipimo sahihi ili kuboresha zaidi na kwenda na teknolojia ya.  

"Pamoja na huduma zake nyingi inazotoa Wakala wa Vipimo,  tunajiita kwenye suala la mizani na uwekaji sticker katika vipimo mbalimbali tunavyovihakiki,"alisema na kuongeza;

 "Kwa kuweka stika, mteja ataiona na hapo itadhihirisha kituo hicho kimehakikiwa na Wakala wa Vipimo na kwamba mahali hapo pamekaguliwa na wakala wa Vipimo,"alisema

Pamoja na hayo Zuberi alizungumzia  Mizani za Kuuzia Mazao ya Wakulima kuwa jitihada za kumlinda mkulima na mfanyabiashara ambapo alisema kuwa Wakala wa Vipimo huhakiki mizani hiyo Kwa kumlinda mlaji na kwamba itamsaidia kujua uhalali wa kipimo husika, kwani baada ya kubandika sticker na Wakala wa Vipimo mlaji atajiridhisha kuwa mizani anayopimiwa bidhaa au kituo cha mafuta anachohudumiwa kimehakikiwa na mamlaka husika (Wakala wa Vipimo).

Hii itasaidia kujua ujazo sahihi wa kitu  husika ambapo walaji watajua kama kipimo kimehakikiwa au hakijahakikiwa

Licha ya hayo alitoa wito kwa wafanyabiashara wote wanaotumia vipimo, kuhakikisha vipimo vyao vimehakikiwa na Wakala wa Vipimo na kuwekewa sticker stahiki na kueleza kuwa suala hilo halina ubabaishaji kwani

Sticker hazifanani (kila sticker ina jina lake kulingana na kipimo) na kila kipimo kina sticker yake.

"Aidha, kwa walaji wote wanaoenda kununua bidhaa kwa kutumia mizani au wanaoenda kwenye vituo vya mafuta kwa ajili ya mahitaji ya mafuta wahakikishe kunakuwa na sticker maalumu kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) ndipo wapimiwe mahitaji yao,"alisema

Kwa upande wake Afisa vipimo mkoa wa Dodoma Said Ibrahim aliwataka wauzaji wa   vipimo kama mizani  wahakikishe wanauza mizani au vipimo vilivyohakikiwa na pia wanunuzi wa vipimo/ mizani wahakikishe wananunua mizani iliyokwisha hakikiwa na wakala wa Vipimo na kuwekewa sticker. 

"Wale wauzaji wa mizani Mkoa wa Dodoma ambao mizani zao zilishahakikiwa na kugongwa muhuri, wafike ofisi yoyote ya Wakala wa Vipimo na risiti zao ili mizani zao ziweze kubandikwa sticker au wawasiliane nasi kupitia simu ya bure 0800110097,"alifafanua Ibrahim .

Alisema kuwa Wakala wa Vipimo ni Taasisi ya Serikali iliyoko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara inayosimamia matumizi sahihi ya vipimo katika biashara, Afya, Usalama na Mazingira.

"Sisi tunasimama Kuilinda jamii kuepukana na madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya vipimo katika Sekta za Biashara, Afya, Usalama na Mazingira,"alisema

Kwa upande wao Rogers Malamsha katibu wa afya hospitali ya DCMC Jijini Dodoma na Philipo Mwalimu wa mazoezi wameshukuru Wakala wa vipimo kutembelea maeneo yao na kufanya ukaguzi na kuahidi kuwa na utaratibu wa kuwaita wakala wa vipimo kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kujiridhisha iwapo mizani wanayotumia iko sawa sawa.



Post a Comment

0 Comments