WIZARA KUNYANGA'NYA HIFADHI ZA WANYAMAPORI ZILIZOGEIZWA KUWA MASHAMBA



 ðŸ“ŒMWANDISHI WETU


WIZARA ya Maliasili na Utalii inakusudia kunyanga'nya maeneo yote ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Jamii ambayo yatakutwa yamelimwa ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na Wanyamapori wakali na Waharibifu .

Hatua hiyo inakuja kufuatia baadhi ya wananchi na viongozi kufanya mashamba na kuanza  kulima mazao ya chakula  katika Hifadhi hizo hali inayopelekea Wanyamapori kama tembo kuacha kula nyasi na kulazimika kutoka nje ya Hifadhi na kwenda  kula mazao hayo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesema hayo leo mapema  Jijini Dodoma  wakati akizungumza na Watendaji wa Wizara hiyo kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya Uhifadhi nchini hususan kwa Wananchi  wanaoishi kando kando mwa maeneo yaliyohifadhiwa.

Amesema kwa mujibu wa sheria maeneo hayo ni mali ya vijiji na yanasimamiwa na Serikali za Vijiji husika na mapato yatokanayo na Hifadhi hizo za Jamii hutumiwa kwa ajili ya manufaa ya Wananchi ikiwemo kuboresha huduma za kijamii kama vile shule na zahanati.

Amesema maeneo hayo ya uhifadhi kusimamiwa na Serikali za vijiji ni ushirikishwaji wa Jamii wa moja kwa moja ili kuiwezesha Jamii kufaidikana uhifadhi wa moja kwa moja

Amesema hatua hiyo ya kunyang'anya itakwenda sambamba na upandishaji hadhi wa Jumuiya hizo za Hifadhi za Wanyamapori za Jamii na kuwa Mapori Tengefu ( Game Controled Area) ambayo kwa mujibu wa Sheria Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) ndiye atakayepewa  kusimamia maeneo hayo.

Akizungumzia hatua hiyo ya kunyang'anya Usimamizi kutoka Serikali za Vijiji na kupelekwa TAWA, Dkt. Ndumbaro amesema kutatuma ujumbe mzito kwa Serikali za Vijiji ambazo zinazosimamia Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori hizo kuwa  zimepewa jukumu la kusimamia Uhifadhi na sio vinginevyo.

Waziri Dkt. Ndumbaro amesema kuna jumla ya  Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori zipatazo 22 na  kati ya hizo ni Jumuiya za Wanyama[pori  10 pekee ndizo zinafanya vizuri kimapato na kiuhifadhi.

Kufuatia hali hiyo, amewataka Wakuu wa wilaya nchini ambao ndio Wenyeviti wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori  nchini  kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kupiga vita shughuli zote za kibinadamu zinazofanyika katika maeneo hayo ambazo haziendani na Uhifadhi.

Nina taarifa ya baadhi ya Jumuiya hizo za Uhifadhi kuna Wakuu wa wilaya ambao ni Wenyeviti wa kusimamia maeneo hayo nao wanalima katika maeneo, hadi kuna wengine wameamua kufungua mashamba ya minazi  katika maeneo ya Wanyamapori hili halikubaliki

Dkt. Ndumbaro.

 

Amesema kuna baadhi ya Jumuiya za Hifadhi za Jamii za Wanyamapori zinazofanya vizuri na zimekuwa zikikusanya pesa nyingi kutoka kwa Watalii ikiwemo Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii ya  Ikona ambayo kwa mwaka inapata bil. 2.6 zinazogawanywa kwa vijiji vitano pekee.

Ametoa wito kwa Serikali za Vijiji kuhakikisha zinasimamia ipasavyo Uhifadhi katika maeneo hayo kwa vile maeneo hayo ni utajiri mkubwa endapo kama yatasimamiwa kwa ajili ya utalii na sio kugeuza kuwa mashamba. 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments