KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE KILIMO,MIFUGO NA MAJI YAPEWA SEMINA KUHUSU NARCO.

 


📌DOTTO KWILASA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imepewa semina kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa malengo ya kujua majukumu yake, muundo wake, utekelezaji wa bajeti, mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto hizo.

Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Msekwa D uliopo ndani ya Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma ambapo viongozi wa Wizara waliongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega.

Akizungumza kuhusu semina hiyo Mhe. Ulega alisema kuwa wizara imeona ni wakati muafaka kufanya semina kuhusu NARCO ili wajumbe wa kamati hiyo waweze kuielewa na kutoa maoni yao ambayo yatasaidia kuboresha   kampuni hiyo na kuleta tija kwa Taifa.

Tunahitaji kuona NARCO  inaendelea kuimarika kwa kuongeza uzalishaji wa mitamba, nyama na kuzidi kuchangia kwenye pato la taifa

Ulega.

Licha ya hayo Ulega alisema kuwa kuna kipindi  Kampuni hiyo ya Ranchi za Taifa ilipita katika kipindi kigumu na hivyo kushindwa kujiendesha lakini kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na wizara kwa sasa Kampuni hiyo inajiendesha yenyewe.

Katika taarifa iliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo, imeainisha mafanikio yaliyopatikana, mipango iliyopo ya kuongeza uzalishaji na maeneo ya vipaumbele yaliyopo katika bajeti ya mwaka 2020/2021. 

Waziri Ulega aliyataja Maeneo hayo kuwa ni Kuboresha Ranchi tano (5) za Kongwa, Ruvu, Kalambo, Missenyi na West Kilimanjaro ili kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo, Kuongeza uzalishaji wa ng’ombe kwa njia ya Uhimilishaji (AI) - kwa kutumia mbegu bora za ng’ombe wa nyama kama vile Boran na Simental.

"Maeneo mengine ni Kudhibiti vifo vya mifugo kwa kiwango kisichozidi 2% ya wastani wa mifugo, Kuongeza na kuboresha nyanda za malisho kwa kudhibiti na kuondoa vichaka na  kuimarisha vyanzo vya maji na Kuweka alama za kuonekana katika mipaka ya ranchi, kuondoa wavamizi na  kuimarisha ulinzi wa mipaka,"alifafanua.

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma alitumia nafasi hiyo kuelezea  muafaka kwa Ranchi hizo na kueleza kuwa  zitaanza kuzalisha malisho kwa ajili ya mifugo ambayo yataweza kuwasaidia hata wafugaji wanaozizunguka ranchi hizo.

 Vilevile alishauri ranchi hizo ziweze kutumika kama mashamba darasa ambapo wafugaji hasa wa maeneo ya jirani wataweza kupata elimu juu ya ufugaji bora.

Akichangia baada ya taarifa kuwasilishwa mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Prof. Patrick Ndakidemi alisema kuwa ni wakati muafaka kwa kamati hiyo kuisaidia NARCO kujiendesha kimkakati kwa kuendana na hali ya Sasa.

 Prof. Ndakidemi alisema, kwa kuwa tayari kampuni hiyo imeshaandaa andiko mradi, ni vema wajumbe hao wakalisoma hilo andiko na kuona ni maeneo yapi kamati inaweza kuisaidia kampuni hiyo.

Vilevile amewasihi NARCO kuendelea kuyatunza na kuyalinda maeneo yao kwani yanawasaidia wafugaji wenye changamoto ya maeneo ya malisho kwa kuwakodishia.

Kwa upande wake Kunti Majala alishauri uongozi wa NARCO kuona namna Bora ya uzalishaji kisasa na kuachana na mazoea hali itakayosaidia kupanuka kwa uzalishaji .

"Tunataka kuona Ranchi zetu zinazalisha nyama bora sio mifugo ambayo haina afya,tunataka kuona na sisi tunasafirisha mazao ya mifugo nje,jaribuni sana kuingia kwa undani kuona namna mtakavyosaidia kutufikisha mbali Zaidi,"alisema Majala.

 

Post a Comment

0 Comments