MAWAZIRI SADC WAPITISHA ITIFAKI YA KUENDELEZA UTALII

 


📌HAPPINESS SHAYO

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)  amesema kuwa itifaki ya kuendeleza utalii imepitishwa na Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanaohusika na Mazingira, Maliasili na Utalii ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi za SADC.

Ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya mkutano wa Mawaziri wa SADC wanaohusika na Mazingira, Maliasili na Utalii uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Amefafanua kuwa Itifaki ya kuendeleza Utalii katika nchi za SADC pamoja na mambo mengine itasaidia kuimarisha shughuli za utangazaji utalii na kupelekea kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi za SADC.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akiongoza mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa SADC wanaohusika na Mazingira, Maliasili na Utalii 


Aidha, Mhe. Mary Masanja amesema kuwa Tanzania kama nchi mwanachama wa SADC imekuwa ikishirikiana na nchi wanachama katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na kufanikiwa kudhibiti ujangili.

Mafanikio yaliyopatikana kutokana na Mkakati wa pamoja wa kudhibiti ujangili ni kukua kwa ushirikiano baina ya nchi wanachama katika kudhibiti ujangili na biashara haramu ya nyara; na ushirikiano kwenye kutoa mafunzo kwa maafisa wanyamaporti kwa lengo la kujenga uwezo katika kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa rasilimali wanyamapori.

Mhe. Masanja.

Naibu Waziri, Mary Masanja amesema kuwa pamoja na mambo mengine mkutano huo Mkutano huu pia umejadili na kupitisha Mkakati wa SADC wa Mabadiliko ya Tabia ya Nchi na Mpango kazi wa utekelezaji wake ambapo nchi wanachama zimehimizwa kuutekeleza mpango kazi huo na zimetaarifiwa kuhusu kuanzishwa kwa Kamati Maalum ya Wataalam kwa ajili ya kuratibu masuala ya mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kupunguza athari za maafa.

Ili kuwezesha kutekeleza jukumu la uhifadhi wa Mazingira, Waheshimiwa Mawaziri tumeridhia Nchi wanachama wa SADC kujiunga na mfuko wa Mazingira ambapo kupitia mfuko huu nchi wanachama zitaweza kupata fedha za ufadhili kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi mazingira

Mhe. Masanja.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Hamad Chande (kushoto) akifuatilia majadiliano



Masuala mengine yaliyojadiliwa na mkutano huo ni Itifaki ya SADC ya Mazingira kwa ajili ya kujenga maendeleo endelevu na Mkakati wa Misitu wa SADC.

Mkutano wa Mawaziri wa SADC hufanyika kila baada ya miaka miwili na nchini Tanzania ulifanyika mara ya mwisho mwaka 2019 Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

 

 

 

Post a Comment

0 Comments