MTAKA AKUTANA NA MALECELA,AMSHIRIKISHA VIPAUMBELE VYAKE

 


📌DOTTO KWILASA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma  Anthony Mtaka,  amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Samweli Malecela ambapo ametumia nafasi hiyo kumshirikisha Mzee huyo vipaumbele vyake katika Mkoa wa Dodoma na kupokea ushauri wa kiongozi na mwanasiasa huyo Mkongwe hapa nchini.

Mtaka amemtembelea Mzee Malecela nyumbani kwake eneo la Uzunguni  Jijini Dodoma, amemweleza Mzee Malecela kuwa kipaumbele chake cha kwanza ni Elimu na kwamba kazi iliyo mbele yake  ni kunyanyua kiwango cha Elimu na Ufaulu katika Mkoa wa Dodoma. 

Ameeleza kuwa Katika kuleta mabadiliko hayo ya Elimu,  atashirikiana na viongozi wazawa wa Mkoa wa Dodoma, wadau wote wenye jukumu la kusimamia elimu kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa hadi Ngazi za Msingi hali kadhalika sekta binafsi.

Ametaja kipaumbele kingine Mtaka alisema atageukia sekta ya kilimo kwa kuzifanya Wilaya za Pembezoni za Mkoa wa Dodoma (Wilaya zinazozunguka Wilaya ya Dodoma) kuwa Kanda Maalum za Kilimo na kukifanya Kilimo cha Mkoa wa Dodoma kuwa cha kibiashara .

Ni nafasi yangu pia kutilia mkazo kwenye zao la Zabibu kama alama ya Mkoa wa Dodoma, Alizeti na mazao mengine ,matumaini yangu ni kuona kilimo kinasaidia kukuza uchumi wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma na kuwa mfano kwa wengine


Licha ya hayo Mtaka amemweleza Mzee Malecela kuwa hali hiyo itasaidia kukidhi  mahitaji makubwa ya mafuta ya chakula ambayo siku za hivi karibuni  ililazimika kuagiza mafuta nje ya nchi.

"Ni  fursa kubwa ya kiuchumi kwa Mkoa wa Dodoma ambao mazao yanayotumika kuzalisha mafuta kama Alizeti, Karanga na Ufuta yanastawi vizuri katika Mkoa wa Dodoma,lazima tutumie nafasi hii kuelekeza nguvu zetu Katika kustawisha mazao haya kwa kuzingatia kanuni Bora za kilimo,"amesema

 Kwa upande wa uboreshaji Mazingira Katika mkoa wa Dodoma, Mtaka aliweka bayana mkakati wake kuwa ataendesha kampeni ya Mkoa ya Upandaji na ustawishaji miti kwa Mkoa Mzima kwa kuwashirikisha Wadau wa ngazi mbalimbali kuanzia Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji, Vitongoji na ngazi za kaya.

"Mzee Malecela naamini utaendelea kunishauri vizuri kwa hili hasa ukizingatia wewe ni mwenyeji wa hapa na unajua hali ya hewa ya mkoa wa Dodoma,nipo tayari kupokea ushauri wako wakati wote ili kufanikisha kupanda miti mingi ili kuendana na azma ya Serikali Katika kuifanya Dodoma kuwa ya kijani,"amesisitiza.

Nae Mzee Malecela ameshukuru kwa mazungumzo yaliyowezesha kubadilishana uzoefu na Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma huku akieleza kuwa Dodoma ina fursa kubwa ya kilimo cha mazao yanayokamuliwa kuzalisha mafuta ya chakula .Amezitaja Wilaya za Kongwa na Mpwapwa kama maeneo yenye hali ya hewa nzuri kwa uzalishaji wa Karanga tangu miaka ya zamani na kwamba maeneo ya Wilaya zingine za Dodoma yanafaa kwa kilimo cha Alizeti na Zabibu.

Pamoja na mambo mengine Malecela amemtaka  Mtaka kuweka mkazo pia kwenye sekta ya ufugaji kwa kutambua Mkoa wa Dodoma una idadi kubwa ya mifugo ambayo ni fursa nyingine ya kukuza uchumi .

Pamoja na Mkoa huu kubahatika kuwa na kituo kikubwa cha utafiti wa mifugo cha Mpwapwa na shamba kubwa la Mifugo la Serikali lililopo Kongwa bado rasilimali hizo hazijasaidia kubadilisha jamii za Wafugaji ,zingatia Sana Katika hili


Malecela.

 


Post a Comment

0 Comments