TANZANIA NA NAMIBIA ZAKUBALIANA KUINUA SEKTA BINAFSI DODOMA

 


📌DOTTO KWILASA

 ILI kukuza na kuendeleza  sekta binafsi nchini,Tanzania na  Namibia  wamekubaliana kuandaa Kongamano litakalofanyika Mkoani Dodoma likihusisha sekta binafsi za pande hizo mbili na maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na pande hizo ili kuona maeneo wanayoweza kushirikiana na kuleta tija kwa nchi hizo.

Hayo yameelezwa  Jijini hapa na Balozi  wa Nchi hiyo  hapa nchini  Lebius Tangeni Tobius alipotembelea ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kufanya nae mazungumzo  ambapo Viongozi hao wawili wamekubaliana kushirikiana kwa maslahi ya pande zote mbili.

Kwa umuhimu huo Serikali  ya Namibia  imesema kuwa  itashirikiana na  Serikali ya mkoa wa Dodoma  kuimarisha  maeneo ya Sekta ya Mifugo, Elimu na Sekta Binafsi  ili kukuza masuala ya uwekezaji na biashara Mkoani hapa.

Balozi huyo amesema,kwa kutambua umuhimu wa kuwa Serikali hizo mbili zina historia ya pekee  katika  mikoa hiyo  miwili ya Omusati na Dodoma  ni vyema kwao kuendeleza mahusiano hayo ya kidiplomasia katika kukuza uchumi wa watu wake .

Amefafanua kuwa ,Mkoa wa Omusati  una sifa na historia ya kipekee kwa kuwa ndio Mkoa ambao chama cha ukombozi wa Namibia cha SWAPO kilizaliwa huku Dodoma ikiwa ni Makao Maku ya Tanzania, makao makuu ya Chama Tawala cha CCM  na Serikali ikiwa imehamishia shughuli zake hapa Dodoma.

Serikali ya Namibia itaendeleza na kuanzisha mahusiano ya kindugu kwa mikoa hii miwili  kwa kutambua kuwa Mkoa wa Omusati una sifa na historia sawa kabisa na Dodoma ,undugu wetu ni hazina tunapaswa kuulinda.

Pamoja na Mambo mengine amesema Katika makubaliano hayo  watashirikiana kwenye eneo la mifugo hususani uongezaji tija ya uzalishaji mifugo na kungeza thamani wa mazao ya mifugo ikiwemo nyama, maziwa na ngozi 

 "Kwa kuzingatia uzoefu tulionao Namibia katika sekta ya mifugo tutashirikiana Katika kuongeza tija kwa mazao ya mifugo ,nadhani hii ni fursa kubwa  kwa Dodoma kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo." aliongeza Balozi huyo wa Namibia.

 Katika kukuza uwekezaji na biashara,  Balozi Tobius wamekubaliana na Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma  Mtaka  kuimarisha mahusiano na mashirikiano kati ya Sekta binafsi ya Namibia na Tanzania hususani katika Mkoa wa Dodoma, ambapo wamekubaliana kuandaa Kongamano litakalofanyika Mkoani Dodoma likihusisha sekta binafsi za pande hizo mbili na maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na pande hizo mbili ili kuona maeneo wanayoweza kushirikiana kwa pamoja.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema kwa Kuwa kipaumbele chake ni kuinua kiwango  Cha  Elimu Mkoani hapa ataitumia  fursa hiyo kwa kushirikiana na Vyuo Vikuu vya Namibia ambapo wataanzisha program za kubadilishana wanafunzi na wataalamu mbalimbali wa vyuo ili kubadilishana uzoefu na utaalamu.

Mbali na hayo Mtaka  ametumia fursa hiyo ya mazungumzo na Balozi Tobius kumualika kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini Tanzania vyenye sifa za kipekee Duniani kama vile Mlima Kilimanjaro, Hifadhi za Taifa za Serengeti na Ruaha ili kupitia yeye awaalike Watalii kutoka Namibia kuja Tanzania.

 Kwa mujibu wa Viongozi hao wawili, Mahusiano kati ya Mkoa wa Omusati Namibia na Dodoma Tanzania yanaendeleza ushirikiano na undugu wa kihistoria uliokuwepo baina ya Tanzania na Namibia tangu enzi za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika ambapo Tanzania ilichangia kwa kiasi kikubwa katika harakati hizo za ukombozi .

Licha ya hayo  viongozi wengi wa harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika waliishi na kupata mafuzo hapa nchini Tanzania.

 

 

 

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments