UKATILI NA MAUAJI YA WAZEE : SERIKALI KUENDELEZA MIKAKATI

 


📌DOTTO KWILASA

SERIKALI imeazimia kuendeleza utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza ukatili na mauaji ya wazee nchini ili kukuza ustawi haki na ujumuishi wazee na hatimaye waishi maisha yenye afya, hadhi na salama.

 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mwanaid Ali Khamis amesema  hayo jana jijini Dodoma wakati  wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wazee.

Amesema kuwa katika kutimiza azma ya kuendelea kuwalinda wazee pamoja na kuimarisha huduma nyingine, serikali ipo katika hatua za mapitio ya sera ya Taifa ya wazee ya 2003, ambayo inaweka msisitizo katika kuimarisha upatikanaji wa haki ya ulinzi na usalama kwa wazee.

Aidha, amesema kuwa sera inayofanyiwa mapitio inalenga kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi katika jamii ya kuwalinda wazee kutokana na hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili, pamoja na mifumo ya upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wazee.

Kutokana na ukweli kwamba hali duni ya kipato ni miongoni mwa sababu zinazochangia vitendo vya ukatili kwa wazee, serikali inalenga kuhakikisha wazee wanawezeshwa katika kubuni na kuendesha shughuli za ujasiriamali kupitia vikundi vidogo vidogo katika jamii ili kuwawezesha kuinua kipato na kumudu mahitaji yao ya msingi

Pia, amesema kuwa wazee watawezeshwa kushiriki katika shughuli za michezo na burudani ili kuimarisha afya zao na kuwajenga kisaikolojia.

Amesema, katika jitihada hizo za kuimarisha ulinzi kwa wazee, serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea na mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee kwa kuongeza msukumo na kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa Mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji ya wazee kwa kipindi cha miaka mitano (2018/2019-2022/2023).

Hata hivyo, amesema kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau, vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee nchini vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.

“Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Polisi, mauaji ya wazee yamepungua kwa kiwango kikubwa kutoka 577 mwaka 2014 hadi wazee 34 Desemba 2020”alisema

Vilevile, alisema kuwa serikali inadhamiria kuongeza jitihada na kuhakikisha mauaji ya wazee yanakwisha kabisa.

“Serikali katika mapitio ya sera ya wazee ya mwaka 2003 imezingatia kuweka msisitizo zaidi katika kuhakikisha wazee wanapata huduma ya msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha ili kusaidia kuimarisha afya na ustawi wao”alisema

Amesema kuwa kwa mujibu wa mwongozo wa kitaifa wa Utoaji wa Huduma za Msaada wa Kisaikolojia wa Mwaka 2021, matatizo mengi ya kiafya na kimahusiano yanayowakabili wazee yanatibika kikamilifu kupitia msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha.

Kadhalika amesema kuwa kupitia Mpango wa serikali wa kuboresha huduma za afya, imeendelea kuhakikisha kuwa kila kituo cha afya cha na hospitali zinakuwa na madirisha maalum kwa ajili ya matibabu kwa wazee.

“Mpaka sasa kuna jumla ya madirisha 2,335 mahususi kwa ajili ya kutolea huduma za matibabu kwa wazee”alisema

Meneja Program, haki na ushirikiano wa wadau kutoka shirika la Help Age Intrnational Tanzania, Joseph Mbasha alisema kuwa shirika hilo ni miongoni mwa mashirika mtandao yaliyopigania utambulisho huo na lina dira ya kuona dunia ambayo kila mzee anaishi maisha yenye afya, hadhi na usalama.

Alisema katika kutekeleza azma hiyo shirika hilo linatekeleza afua tano, ambazo ni kuboresha upatikanaji wa huduma za afya zilizo rafiki na bora kwa wazee.

Alisema afua nyingine ni kupinga vitendo vya ukatili na manyanyaso dhidi ya wazee, kutoa huduma jumuishi wakati wa majanga, kuhakikisha usalama wa kipato, pamoja na kuchagiza harakati za mabadiliko.

Kutokana na hayo ,Tume ya haki za binadamu na Utawala bora(THBUB)imesema kuwa kunahitajika kuwekwa kwa mifumo madhubuti ya kulinda na kutetea haki za makundi maalum yanayohitaji ulinzi wa jamii husika.

Akitoa salamu za Tume hiyo , Kamishna wa THBUB,   Dkt. Fatma Khalfani kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu, katika Maadhimisho hayo alisema kuwa Katika kutekeleza suala hili nchini,Ibaraya12(2)na Ibaraya14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano waTanzania ya mwaka1977 pamoja na  marekebisho yake,zimeeleza juu ya wazee kupewa heshima na kupata hifadhi kutoka kwa jamii wanamoishi.

Dkt.Khalfani aliongeza kuwa heshima kwa wazee kwenye jamii zetu nyingi za kiafrika na Tanzania imekuwa ikipewa kipaumbele na mara zote wazee wamekuwa sehemu ya familia.

Kutokana na umuhimu huo alisema,Tume inawasihi wadau wote kuenzi na kudumisha utamaduni huo kwa kutekeleza wajibu wao,ikiwemo kuwapatia wazee ulinzi na usalama,chakula,malazi na mavazi.

"Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002,Tanzania ilikuwa na wazee 1,952,041(sawa na wanaume 940,229 na wanawake 1,011,812)na katika sensa ya mwaka 2012 idadi ya wazee ili ongezeka hadi kufikia 2,507,568(wanaume1,200,210 na wanawake1,307,358) sawana5.6%ya wananchi wote,"alisema.

 

Post a Comment

0 Comments