WAZIRI MKUU AIPONGEZA BENKI YA CRDB KWA KUANDAA BONANZA LA MICHEZO DODOMA



📌ALEX SONNA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa bonanza la michezo lililopewa jina la “CRDB Bank Pamoja Bonanza” ambalo pamoja na kuhamasisha utamaduni wa kushiriki katika michezo na kujenga afya pia linalengo la kuhamasisha mshikamano kwa Watanzania na ushiriki katika shughuli za maendeleo.

Pongezi hizo amezitoa leo Juni 12,2021   wakati wa  Bonanza la Michezo lililoandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu “CRDB Bank Pamoja Bonanza” lililofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Waziri Mkuu amesema kuwa bonanza hilo linatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ya kuwaleta Watanzania pamoja na kushirikiana katika shughuli za kijamii na uchumi wa Taifa letu.



“Mhe. Rais katika moja ya hotuba zake alituasa tukitaka kwenda haraka twende peke yetu, lakini tukitaka kwenda mbali twenda pamoja. Asanteni Benki ya CRDB kwa kuonyesha mfano wa kutuleta pamoja Bunge, Wizara pamoja na Wananchi wote kupitia CRDB Bank Pamoja Bonanza,” amesema Waziri Mkuu.

Aidha, Waziri Mkuu amezitaka taasisi nyengine za umma na binafsi kuiga mfano wa Benki ya CRDB kwa kuandaa mabonanza kama hilo ilikuendelea kujenga utamaduni wa michezo na mshikamano miongoni mwa Watanzania. “Niwahamasishe na Watanzania kuendelea kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya zetu,”amesisitiza

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuwa lengo kuu la kuandaa bonanza hilo ni kuisogeza benki hiyo karibu na Serikali, Bunge na Wizara, ili kupata nafasi ya kusikiliza mahitaji yaliyopo na kujua namna gani benki hiyo inaweza shiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya nchi.

Miaka ya nyuma tulikuwa tukifanya bonanza hili na Bunge, mwaka huu tumeshirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kushirikisha Wizara zote. Malengo yetu mwakani ni kuhusisha muhimili mwengine wa Serikali kwamaana ya Mahakama.

Nsekela.

Naye Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dkt. Tulia Ackson ameiomba Benki ya CRDB kuendeleza utamaduni huo ambao wamekuwa nao kila mwaka Wa kushirikiana na Bunge katika kuhamasisha michezo na kujenga mahusiano. “Tunawapongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa bonanza hili kwa mara nyengine tena, hii ni njia nzuri sana ya kujenga mahusiano huku tukiimarisha afya zetu.




Akikabidhi kombe na medali kwa mshindi wa jumla Benki ya CRDB, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amewapongeza washindi katika bonanza hilo na kuwashukuru watumishi wote wa Serikali, Bunge, Benki ya CRDB na wananchi waliojotokeza kushiriki katika bonanza hilo.

 Katika CRDB Bank Pamoja Bonanza, timu ya Benki ya CRDB iliibuka mshindi katika mpira wa miguu, timu ya Bunge iliibuka mshindi katika mpira wa kikapu na katika mpira wa pete timu ya Watumishi wa Wizara iliibuka mshindi.

Vilevile kulikuwa na michezo mingine ya burudani ikiwamo kuvuta Kamba, kukimbia na magunia, kufukuza kuku, mchezo wa bao, karata, draft, pamoja na pool table.












Post a Comment

0 Comments