📌BENNY MWAIPAJA
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni,
ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itekeleze haraka maelekezo yaliyotolewa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi
karibuni kuhusu Taasisi za Fedha kupunguza riba za mikopo ili kuwawezesha
wafanyabiashara na watanzania kwa ujumla kukopa na kuendeleza shughuli zao za
kiuchumi.
Mhe. Masauni ametoa maagizo hayo alipotembelea Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) Jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Benki hiyo ikiwa
ni mwendelezo wa ziara zake za kutembelea Taasisi zilizochini ya Wizara ya
Fedha na Mipango.
Alipongeza jitihada zinazofanywa na Benki Kuu ya Tanzania za kukutana na
wadau ili kuhakikisha kuwa Taasisi za Fedha zikiwemo Benki na Watoa huduma wa
Sekta Ndogo ya Fedha wanapunguza riba za mikopo yao ili kuwawezesha wananchi
kupata mikopo isiyo na gharama kubwa.
Niwapongeze kwa juhudi zilizoanza kuchukuliwa kuwezesha riba kupungua na ikiwezekana mwishoni mwa mwezi huu wananchi waanze kuona matokeo ya juhudi hizo kwa riba kuanza kupungua, kwa kuwa kupungua kwa riba ni jambo linalowezekana
Mhandisi Masauni.
Aidha, ameitaka Benki hiyo kuhakikisha inaweka mikakati mahususi ya
kuongeza akiba ya Fedha za kigeni kwa kuwa na mbinu za kibunifu zikiwemo kuanza
kununua na kuhifadhi dhahabu pamoja na kuongeza uuzaji wa bidhaa za Tanzania
nje ya nchi na kusimamia kikamilifu shughuli za utalii.
Kuhusu suala la fedha za wananchi waliokuwa wateja wa Benki ya FBME Limited iliyowekwa chini ya uangalizi wa Bima ya Amana za Wateja inayosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania ikiwa katika hatua za kufilisiwa, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Yussuf Masauni, ameitaka Benki hiyo kuhakikisha wateja wa Benki hiyo wanarejeshewa fedha zao haraka baada ya kukamilisha taratibu za kisheria zinazoendelea nchini Cyprus.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Bernard Kibesse, akifafanua jambo |
Kwa upande wake Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt.
Bernard Kibesse, alimhakikishia Mhe. Naibu Waziri Masauni kwamba Benki yake
inakamilisha mazungumzo na mabenki ili washushe riba kama alivyoelekeza
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza.
Alisema Benki Kuu pia inaendelea kurekebisha kanuni mbalimbali za mikopo
inayotolewa na Benki hiyo kwa Mabenki ili kuziongezea ukwasi Benki hizo ili na
zenyewe zitumie fursa hiyo kushusha riba za mikopo.
Aidha, Naibu Gavana Dkt. Kibese alieleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania
itaanza kununua na kuhifadhi dhahabu baada ya Kiwanda cha kuchakata dhahabu cha
Mwanza kilichozinduliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza
hivi karibuni kupata hati ya uthibitisho ya uzalishaji wa dhahabu wa viwango
vya kimataifa ambavyo ili cheti hicho kitolewe, kiwanda kinatakiwa kuzalisha
dhahabu yenye ubora wa asilimia 99.9.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Masauni yupo jijini Dar es
Salaam katika ziara yake kikazi ambapo atatembelea ofisi zilizo chini ya Wizara
ya Fedha na Mipango.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (wa tatu kulia), Manaibu Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dkt. Bernard Kibesse na Bw. Julian Banzi Raphael, wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Benki hiyo, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam) |
0 Comments