📌DOTTO KWILASA
MKUU wa Mkoa wa
Dodoma,Anthony Mtaka ameisimamisha Kampuni ya upimaji Ardhi ya GEOPLAN Ltd kufanya shughuli zake na badala yake kazi
yake itafanywa na timu ya wataalamu wa Ardhi kutoka Jiji.
Hatua hii imekuja kufuatia
baadhi ya wananchi wa Michese Kata ya Mkonze Jijini Dodoma kuilalamikia
kampuni hiyo ya upimaji ardhi kutoa
Lugha za kuudhi pindi wananchi wanapohitaji maelezo kutoka kwao Pamoja na
kuwadhulumu maeneo yao na kuyauza kinyume na taratibu.
Mtaka ametoa uamuzi huo Jijini hapa mara baada ya kusikiliza
kero za wananchi wa eneo hilo kuhusiana na suala la upimaji wa Ardhi huku akiagiza kazi ya upimaji kufanywa na
Wataalam wa Jiji la Dodoma pamoja na
Wizara ya Ardhi,Nyumba na maendeleo ya makazi.
Aidha amewataka wananchi hao kuwa watulivu na kuendelea kuheshimu maeneo yaliyopimwa bila kutofanya
chochote hadi hapo uongozi wa Jiji na Wizara ya Ardhi watakapoenda kusuluhisha
migogoro hiyo.
Mbali na hayo Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma ametumia nafasi
hiyo pia kuwaelekeza Wafanyakazi na wataalamu wa Ardhi Jijini hapa kuwa na
Lugha nzuri wanaowahudumia wananchi.
Amesema baadhi ya wataalamu wa Ardhi wa jiji wamekuwa na
kauli chafu na zinazoudhi kwa wananchi hali inayosababisha suala la migogoro ya
ardhi kuendelea kuwa sugu.
"Nawaombeni sana acheni kutoa lugha mbaya kwa wananchi
wanapohitaji huduma,jaribuni kuwaelekeza kwa kuwaheshimu na hii itasaidia
kumaliza migogoro mapema,"amesema na kuongeza;
"Jaribuni sana kuwa na heshima kwa kila mtu,kabla
hujaanza kumhudumia mwananchi mchukulie Kama baba au mama yako aliyeko huko kijijini
kwenu,"amesisitiza Mtaka.
Awali wakielezea kero zao baadhi ya wakazi hao wa michese
wamesema kuwa wanashangazwa na kitendo cha Kampuni hiyo ambayo imekuwa ikipima
maeneo hayo na kujimilikisha kinyume
na taratibu.
“Mkuu wa mkoa bora umekuja najua utatusaidia kwasabu
tumenyanyasika kwa muda mrefu na hii kampuni, sisi hatuitaki kwasababu imekuwa
haitutendei haki licha ya kutupimia maeneo lakini imekuwa ikijimilikisha maeneo
mengine”,walisema.
Wamesema kuwa licha ya wao kuwa na kamati ya usimamizi wa
Kampuni hiyo katika eneo la Michese hakuna kinachofanyika zaidi ya kuchukuliwa
maeneo yao jambo ambalo wamesema sio haki.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri amesema
kuwa asili ya mgogoro wa eneo hilo ni
kutokona na upimaji na urasimishaji wa eneo na hivyo kupelekea malalamiko hayo na kuamua kuja na uongozi wa
Mkoa ili kusikiliza kero za wakazi wa Michese.
Kutokana na kuwepo kwa migogoro ya Ardhi katika Jiji hilo
tayari Wananchi wengi wamefikiwa na zoezi la usikilizaji wa kero tangu Julai5
hadi julai16 kwa Kamati inayosikiliza migogoro hiyo ambapo tayari imepokea jumla ya
migogoro2382kati ya hiyo zaidi ya migogoro500 imetatuliwa huku zikiongezwa
siku10 kwaajili ya utatuzi wa migogo ya Ardhi Jijini Dodoma.
MWISHO
0 Comments