PROFESA MKENDA AYATAKA MABENKI KUSHUSHA RIBA KWA WAKULIMA KUWEZESHA KILIMO CHA ALIZETI

 


📌PENDO MANGALA

WAZIRI wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda ameyataka Mabenki nchini kushusha riba kwa wakulima ili kuweza kusaidia  kilimo Cha alizeti kutokana na uhitaji wa mafuta ya kula nchini hivi sasa kuwa mkubwa.

Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo hii leo Jijini Dodoma wakati alipokuwa akifunga wiki ya Taasisi ya Pass Trust ambayo inajishughulisha na kuwawezesha wakulima na wajasiriamali katika utoaji wa mikopo ili wajikwamue na umaskini.

Aidha amesema kutokana na kuwepo kwa uhitaji wa mafuta ya kula nchini  endapo mabenki hayo yatapunguza riba kwa wakulima yataiwezesha nchi kujitosheleza kwa mafuta ikiwa ni pamoja na kuuza nje ya nchi na kuongeza pato la Taifa.

Sanjari na hilo amesema  Serikali inatarajia kugawa mbegu za Alizeti kwa wenye viwanda kwa mkataba lengo likiwa ni kumsaidia mkulima ili aweze kuzalisha kwa tija.

Hivi sasa kuna  uhaba wa mbegu na hivyo kukosa tija na namna ya kulima na hivyo imefikia hatua tunaagiza mafuta ya mawese Malaysia hali ambayo inasababisha Vijana wetu kukosa ajira

Pamoja na mambo mengine amesema lengo la Serikali kugawa  mbegu kwa  Wenye viwanda kwa mkataba ili iingie mkataba na wakulima wakubwa au vyama vya ushirika na baadae watalazimika kuwakabidhi wakulima bila malipo. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka amesema Serikali inatarajia kusajili Kaya 300,000. zinazostahili kufanya kilimo cha Alizeti na  zao la zabibu .

Sisi kwa nafasi yetu Kama Mkoa tutashauriana na Wizara ya kilimo kuona namna ya kuhudumia  zao la zabibu ili kuwa na kilimo biashara kwa lengo la kuongeza pato la Taifa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi ya PASS TRUS Tausi Akida amesema kuwa changamoto za mitaji bado zipo na kusema kuwa ipo haja kwa Taasisi za fedha kuongeza kiwango cha kilimo na kwamba katika mikopo ya trilioni 19 iliyotolewa Shilingi Trilioni 1 ndio zilienda kwenye kilimo.

“Suala hili bado ni muhimu ili kuweka tija kwani Mazao ya kimkakati PassTrust  imeshiriki Katika kukuza zao la alizeti na zabibu kwa kusapoti viwanda vya uchakataji kwa kuwawezesha mitaji ambapo tumekuwa tukiwaunganisha na mabenki ambayo huwa yanawapa mikopo,”amesema.

Hata hivyo  amesema hivi sasa wameanza na programu ya kutoa zana za kilimo kwa wakulima na programu hiyo ipo katika Mikoa  ya Simiyu,Dodoma,Singida na Morogoro.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments