📌PETER HAULE,
WFM.
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamadi Yussuf Masauni,
amekiagiza Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA)
kufanya tafiti zitakazo ibua vyanzo vipya vya mapato na kodi ili kuisaidia
Serikali katika kutekeleza mipango ya maendeleo kwa watanzania.
Agizo hilo limetolewa jijini Dar es Salaam
alipotembelea Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Uhasibu Tanzania
(TIA) ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya vyuo hivyo
katika mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zote zilizo chini ya
wizara hiyo.
Mhandisi Masauni alisema kuwa Vyuo hivyo vimekuwa vikifanya vizuri
katika mambo ya taaluma kwa kuongeza Kozi mbalimbali, idadi ya wanafunzi licha
ya changamoto ya miundombinu na ufaulu lakini suala la utafiti linatakiwa pia
kupewa msukumo wa ziada.
Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2021/22 imepokelewa vizuri na wabunge na wananchi kwa ujumla hususani katika mabadiliko ya kodi na vyanzo vya mapato, lakini jambo hili linaweza kuwa endelevu kwa kufanya tafiti zaidi ili kuweza kuwa na kodi na vyanzo vipya vya mapato ambavyo si kero kwa mwananchi.
Mhandisi Masauni.
Mhandisi Masauni amevitaka Vyuo hivyo kuendelea kufanya tafiti pia
katika eneo la ununuzi na ugavi na kutoa ushauri kwa Serikali ili kuongeza
nguvu katika usimamizi wa fedha za miradi kwa kuwa fedha nyingi hutengwa kwa
ajili ya maeneo hayo.
Amezihakikishia Menejimeti za Vyuo hivyo kuwa Wizara ya Fedha na Mipango
itashirikiana navyo kufanikisha tafiti zitakazoongeza tija kwenye uchumi na
maendeleo ya nchi.
Mhandisi Masauni alisema kuwa Vyuo hivyo vinawataalamu wabobezi katika
masuala ya usimamaizi wa fedha na bima, masuala ya ugavi na ununuzi hivyo
wanaweza kuwa washauri wazuri katika nyanja hizo kwa Wizara ya Fedha na Mipango
iliyopewa dhamana ya kusimamia uchumi wa nchi na Serikali kwa ujumla ili kuweza
kupiga hatua za maendeleo.
Alisema kuwa suala la ushauri elekezi unaotokana na tafiti una tija si
tu kwa mapato ya Serikali lakini pia kwa vyuo, hivyo ni vema Vyuo hivyo
vikaongeza jitihada za kuongeza tafiti na ushauri kwa Serikali kwa kuwa kuna
uhitaji mkubwa.
Aidha amevitaka Vyuo hivyo kutoa mafunzo ya muda mfupi hususani kwa
watumishi wa umma wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazofanana na fani zilizopo
katika Vyuo hivyo ili kuwaongezea uwezo lakini pia kukuza kipato cha chuo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), Dkt. Momole
Kasambala, alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2019/20 hadi sasa taasisi
imefanikiwa kuboresha miundombinu ya utafiti, ushauri wa kitaalamu na
machapisho.
Dkt. Momole alisema kuwa TIA imefanikiwa kutoa ushauri wa kitaalamu
kuhusu mbinu za ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa
Halmashauri tano hadi kufikia, Juni 2021.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Prof. Tadeo
Satta, amesema kuwa idadi ya tafiti imeongezeka na sasa wameingia katika hatua
ya uandishi wa vitabu na pia suala la mafunzo kwa watumishi wa umma litafanyiwa
kazi ili kuongeza tija katika utendaji kazi kwa waTumishi wa umma.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni |
Wakuu wa Vyuo hivyo wamemshukuru Naibu Waziri Mhandisi Hamad Yussuf
Masauni, kwa kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili
kuona majukumu yanatekelezwa kwa ufanisi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Masauni, anaendelea na ziara
ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, jijini Dar es Salaam.
0 Comments