WATUMISHI 473 WAITWA KAZINI WIZARA YA AFYA

 


📌DOTTO KWILASA

SERIKALI imewaita kazini watumishi wa kada ya afya waliopo chini ya Wizara ya Afya wapatao 473 kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na watumishi mbalimbali kufariki,kukoma utumishi na kustaafu.

Hatua hiyo imekuja kufuatia Wizara hiyo kutoa kibali Cha ajira mbadala za kada mbalimbali za Afya Kupitia tovuti ya Wizara mnamo Mei 12 Mwaka huu zilizotokana na watumishi kukoma utumishi kutokana na sababu mbalimbali. 

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Profesa Abel Makubi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ajira hizo huku akisisitiza kuwa watu hao wameitwa kutokana na kukidhi vigezo vya ajira.

Watumishi  waliochaguliwa watakuja kujaza nafasi zilizoachwa wazi na watumishi mbalimbali ambao walistaafu,waliofariki na wengine kuacha kazi.

Prof.Abel Makubi

Hata hivyo amefafanua kuwa kutokana na nafasi hizo 473 zilizotangazwa na Wizara hiyo,walipokea jumla ya maombi 19757 ambapo  kati ya hayo maombi 4760 yalikosa sifa kutokana na kutokamilisha taratibu za uombaji.

"Wengi hawakukamilisha taratibu za uombaji kwa kushindwa kuambatanisha vyeti vya taaluma huku Baadhi wakiomba nafasi ambayo sio taaluma yao hivyo  maombi yao  kutokidhi vigezo,hivyo basi maombi 9338 ndiyo  yamekidhi vigezo na sifa  za kuajiriwa,"amefafanua.

Sambamba na hayo Prof.Makubi ameeleza vigezo vilivyotumika kuwapata waombaji hao Kuwa ni Pamoja na kuzingatia waombaji wenye ulemavu,wenye ajira za mikataba ya muda,waombaji wenye umri chini ya miaka 45 na waombaji waliohitimu elimu ya Mwaka 2018 na kurudi nyuma.

Kwa umuhimu huo amefafanua pia mgawanyo wa nafasi hizo 473 kwa kada mbalimbali kulingana na walivyopokea kutoka Ofisi-Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora kwamba katika kada ya Daktari bingwa idadi ya nafasi zilizohitaji kibali ni Saba na waliochaguliwa ni Saba.

Daktari daraja la pili 23,Daktari wa meno 5,Afisa Muuguzi 17,Afisa Muuguzi msaidizi 67,nafasi ya Muuguzi 140,Afisa afya mazingira 3 na Afisa afya mazingira msaidizi 3.

Prof.Abel Makubi

Licha ya hayo amezitaja nafasi nyingine za Fundi sanifu vifaa tiba nafasi 1 , Fiziotherapia nafasi 2,Katibu wa afya 1,Famasia 7,Mteknolojia-Meno 3,Mteknolojia-Mionzi 5,Mteknolojia Maabala 10 ,Myeknolojia-Macho 5, Mteknolojia Msaidizi Maabala 8 Pamoja na Msaidizi wa afya 166.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amewataka waliochaguliwa katika nafasi hizo kuripoti katika Hospitali ya Mirembe Jijini Dodoma kuanzia leo hadi Julai 9 Mwaka huu wakiwa na nakala halisi pamoja na vivuli vya vyeti.

 

Post a Comment

0 Comments