WIZARA YA KILIMO YATANGAZA MIKAKATI KUDHIBITI BEI YA MBOLEA



📌DOTTO KWILASA

SERIKALI imewashauri wakulima kutumia mbolea aina  ya NPS na NPS ZIN-N.K  kupandia mazao ambapo gharama yake inatajwa kuwa ni ahueni ikilinganishwa na mbolea ya DAP ambayo hutumiwa na wakulima wengi huku bei yake ikiwa juu kwenye soko la  dunia na kuwa kikwazo kwa wakulima wa hali ya chini.

Hatua hii imekuja  kutokana na malalamiko mengi ya wakulima kushindwa kumudu gharama za mbolea na kusababisha kushindwa kuendeleza kilimo ambacho ndiyo uti wa mgongo wa Taifa huku ajira nyingi za vijana zikitokana na sekta hiyo. 

Akizungumza na waandishi wa habari  Jijini hapa, Waziri wa Kilimo Prof.Adolf Mkenda amesema mbolea zote hizo za aina tatu zinatumika kupandia mazao lakini kwa sababu moja kati ya hizo  gharama yake iko juu  wakulima wanapaswa kutumia inayoendana na hali yao kiuchumi.

Amefafanua kuwa Mbolea ya DAP kwenye madukuka ya Dar es Salam Kg 50 inauzwa sh. 75,000 na bei yake inaongezeka  kwa mikoani hadi kufikia  100,000 bei ambayo inawaelemea wakulima.

Amesema”Tumezungumza na watu wanaoagiza mbolea ya NPS na NPS-ZINK   ambao shehena wanayo na wataongeza nyingine   ambayo watauza 60,000 kwa mfuko wa kg 50 ambayo ni sawa na bei ya mbolea ya mwaka jana na kwa sababu mbolea ni ya kutosha tunahakikisha bei ya aina hii ya mbolea haitapanda tena,”amesema.

"Hatua nyingine tutahakikisha mbolea inayokuja nchini ikifika bandalini inashushwa mapema na kupelekwa kwenye maeneo husika hali hiyo itasaidia kupunguza gharama za bandarini ambazo zilikuwa zinasababisha kuongeza gharama ya mfuko wa mbolea,"amefafanua.

Mbali na hayo amebainisha kuwa Wizara hiyo imeamua kukutana na wafanyabiashara wa mbolea  nchini kwa lengo la kukubaliana kuagiza mbolea kwa pamoja ili kupungiza gharama za usafirishaji.

“Nampongeza waziri anayehusika na mamlaka ya bandari kwa kutuhakikishia kuwa mbolea inapofika bandarini haicheleweshwi,unapoagiza mzigo mkubwa wa mbolea hata gharama inapungua na kutoa kibali kwa mamlaka ya mbolea kutoa vibali vya uagizaji mbolea ili wadau wengi waweze kushawishika na kuagiza,”amesema Mkenda.

"Wakulima wasiwe na hofu kwani serikali ni sikivu na itahakikisha inafanya kila jitihada ili wakulima waendelee kuzalisha,"amesema.

Kutokana na hayo,Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo(TARI) Cha Mlingano Tanga  Catheline Senkoro amesema mbolea ya  NPS na NPS-ZIN-N.K  tayari imeshafanyiwa utafiti na inafanya vizuri na tayari imeonyesha matokeo chanya kwenye mikoa ya nyanda za juu kusini.

Ameongeza kuwa "Wakulima wengi wamezoea kutumia mbolea ya aina moja ya DAP ambayo kwa sasa bei yake iko juu na wakulima wengi watashindwa kumudu gharama,nawatoa hofu wakulima mbolea hizi ni nzuri na zimefanyiwa  utafiti kwenye mikoa ya iringa, njombe na songwe,"amesema


Post a Comment

0 Comments