DKT. NDUMBARO: HAKUNA UTHIBITISHO PEMBE ZA FARU KUONGEZA NGUVU ZA KIUME,MSIWAUE

 

Dkt. Ndumbaro (tano kutoka kushoto) akiwa na Wajumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Wadau wa Utalii  wakishuhudia zoezi la  uzinduzi wa uwekaji wa alama za utambuzi wa faru katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. 


📌MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameitaka Jamii kuachana na imani potofu kuwa pembe za faru zinaongeza nguvu za kiume kwani hakuna uthibitisho wa kisayansi juu ya madai hayo baadala yake ameitaka Jamii kuungana na Serikali katika kumlinda faru ambaye ni kivutio kikubwa cha utalii hapa nchini.

 Amesema kutokana na imani hiyo potofu  imepelekea  faru kuwindwa sana na kuna baadhi ya nchi zimekuwa zikinunua pembe  hizo za faru kwa bei ya ajabu, hali hii imeilazimu Serikali ya Tanzania kujizatiti katika  kuwalinda faru kwa kuwawekea vifaa maalum ajili ya ulinzi ili wasiweze kuuawa

Ametoa kauli hiyo wakati akizindua zoezi la uwekaji wa alama pamoja na vifaa maalum kwa faru katika Mamlaka ya  Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa Wanyama hao ambao ni zao kubwa la Utalii nchini

Dkt.Ndumbaro amesema kuhifadhi faru kunataka nguvu ya ziada pamoja na  akili ya ziada kwa sababu binadamu ni kiumbe mharibifu na tayari ameingiza mawazo yake  kuwa nyara zina nguvu ya ziada.

Kufuatia hali hiyo  ameaugiza Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ushirikiane na  Idara ya  Wanyamapori kuhakikisha wanakamilisha kuweka alama na vifaa  maalum kwa ajili ya utambuzi na ulinzi  kwa faru wapatao  45  badala ya kuwawekea vifaa hivyo  faru 20 pekee waliokuwa wamepanga kuanza nao  lengo likiwa ni kuhakikisha faru wote  katika eneo hilo wanakuwa salama zaidi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ( wa nne kulia) akipewa maelezo kutoka kwa Kamishna Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kabla ya kuanza kwa zoezi la  uzinduzi wa uwekaji wa alama pamoja na vifaa maalum kwa ajili ya utambuzi na kufatilia nyendo za faru 

Dkt.Ndumbaro ameeleza kuwa  faru wote wanatakiwa kuwekewa vifaa hivyo kwa sababu wale 25 kati ya 45  ambao watakuwa wamesalia wanaweza kukutana na balaa yoyote

 Ambapo ameutaka Uongozi wa Hifadhi ya Ngorongoro kama una changamoto yyoyote wamfikishie ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa faru wote kwa sababu mitambo iliyopo ina uwezo wa  kufuatilia nyendo za faru zaidi ya 100,000 kwa ajili ya usalama wao.

 Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro ameuagiza Uongozi wa Hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha faru wenye watoto wadogo wanahifadhiwa katika maeneo maalum hadi pale faru wadogo watakapokuwa wakubwa  ndipo waweze  kurudishwa katika mazingira yao asili ili wasiweze kuliwa na fisi

Kwa mujibu wa taarifa  fisi wamekuwa tishio kubwa kwa watoto wa faru ambapo faru wanapokuwa wadogo wamekuwa wakiliwa na fisi ambapo katika eneo la Ngorongoro kuna  idadi kubwa sana ya fisi 

Amefafanua sababu za kuliwa na faru wadogo ambapo amesema  faru wenye watoto  wadogo huliwa kwa sababu faru weusi kiasili huacha watoto wadogo  nyuma wakati wa kutafuta malisho hivyo fisi hutumia nafasi hiyo kuvamia na kuwala watoto hao.

Amesema kutokana na umuhimu wa fisi kiikilojia na kiutalii haiwezekani kuwaondoa fisi  ila jambo linalotakiwa kufanywa  ni kuhakikisha faru watoto wanalindwa kwa kuwaondoa katika mazingira hayo hatarishi.

Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro ameagiza Uongozi wa Hifadhi hiyo kutenga eneo maalum kwa ajili  faru wazee ambao kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu kuwa faru wanapozeeka hupoteza uwezo wa kuona  hivyo litengwe  maalum kwa ajili ya kuwahufadhi faru hao ili litumike kwa ajili ya  utalii wa faru.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ( katika ) akiwa kwenye picha ya  pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Wadau wa Uhifadhi nchini  mara baada ya kushuhudia  zoezi la  uzinduzi wa uwekaji wa alama pamoja na vifaa maalum kwa ajili ya utambuzi na kufuatilia nyendo

Awali, Kamishna Uhifahi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro , Dkt.Freddy Manongi amesema Ngorongoro ni eneo pekee dunia ambalo watalii wataweza kumuona faru weusi katika mazingira yake asilia

Aidha, Dkt.Manongi amueleza changamoto wanazokabiliana katika kumlinda faru kutoka na ûwepo matumizi mseto katika eneo hali inayochangia katika kuwalinda faru  hao.

Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Maurus Msuha ameeleza kuwa zoezi la kuweka alama kwa Faru ni utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopatikana faru yanalindwa kwa mbinu za kisasa na faru hao  kuwekewa alama za utambuzi ili kuwafuatilia mienendo yao kwa urahisi zaidi.

 

Post a Comment

0 Comments