WADAU WATOA MAONI MAREKEBISHO YA KANUNI ZA SHERIA YA EPOCA

 


 ðŸ“ŒFARAJA MPINA NA COLNELIA MUNYI

SERIKALI imewakutanisha wadau wa Sekta ya Mawasiliano na Habari kujadili na kutoa maoni kwenye rasimu ya marekebisho ya kanuni nne za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA). Kanuni hizo ni kanuni za leseni, kanuni za maudhui mtandaoni, kanuni za miundombinu ya utangazaji kidijitali na kanuni za maudhui ya redio na runinga

Akifungua kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Serikali imeona umuhimu wa kuwaita wadau hao ili kupata maoni yao kwasababu wao ndio watekelezaji wa kanuni hizo



Dkt. Yonazi amezungumza na wadau hao na kuwaeleza kuwa matamanio ya Serikali ni kuboresha mazingira ya watoa huduma za mawasiliano na habari nchini ili wananchi waweze kunufaika na kufaidi bidhaa na huduma bora za mawasiliano

Ameongeza kuwa hadhira hiyo imekutana kwa ajili ya kufanya maboresho ya kanuni hizo kwa kutoa maoni yao katika maeneo ambayo yamefanyiwa mapitio hivyo ushirikiano wao na mchango wao unahitajika ili kufikia malengo yaliyokusudiwa

Naye Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Philip Filikunjombe amesema kuwa maboresho ambayo wadau wanatolea maoni yanaenda kuleta mabadiliko katika Sekta ya Mawasiliano na Habari kwa kutenganisha kati ya watoa huduma za maudhui mtandaoni kama chombo cha habari na wale wanaotoa maudhui ambayo hayahusiani na vyombo vya habari



Amesema kuwa maboresho hayo yataenda kutatua sintofahamu ya nani anatakiwa kupatiwa leseni ya kuweka maudhui mtandaoni pamoja na kushusha ada ya leseni hizo kwa mwaka ambapo maombi ya leseni kwenye rasimu ya hiyo imeshuka kutoka shilingi laki moja hadi 50,000/= na ada ya leseni kwa mwaka imeshuka kutoka shilingi milioni moja hadi shilingi laki 5 kwa mwaka

Aidha amezungumzia kanuni zilizopo kwa sasa zinawataka watoa huduma wa redio na runinga kuomba leseni ya kutaka maudhui yaleyale kuonekana mtandaoni lakini rasimu hiyo ya maboresho ya kanuni hawatatakiwa kuomba leseni tena ili vipindi vyao kuonekana kupitia mtandao

Dkt. Filikunjombe amezungumzia maboresho ya kanuni hizo kuwa yanaenda kupunguza ada ya leseni ya kurusha matangazo ya redio na runinga kwa asilimia 30 na kuruhusu vituo vya redio na runinga kujiunga na vituo vingine kurusha maudhui yao bila kupata kibali kutoka TCRA isipokuwa watatakiwa kupeleka mpangilio wa vipindi unaoonesha kuwa atajiunga na kituo kingine

Amesema kuwa maboresho hayo yanaenda kuhakikisha ving’amuzi vyote vinaonesha chaneli za bure bila kujali ni king’amuzi cha kulipia au la ili kuongeza wigo wa wananchi kupata taarifa

Maboresho mengine yaliyofanyika ni katika vipengele vya matangazo ya mubashara na kuruhusu runinga za kulipia kuchukua matangazo na kubadili leseni ya redio na runinga za jamii kutoka leseni kubwa kwenda kuwekwa kwenye kundi la leseni ndogo



Aidha, wadau mbalimbali walitoa maoni kuhusu rasimu ya kanuni hizo kwa makundi wakiwemo wadau kutoka Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CORI), Baraza la Habari Tanzania (MCT), MISA Tanzania, Umoja wa Makampuni ya Simu Tanzania (TAMNOA), Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Wamiliki wa Ving’amuzi na Jukwaa la Wahariri Tanzania

Kanuni nne zilizofanyiwa maboresho ni miongoni mwa kanuni 22 za mawasiliano na utangazaji zinazosimamiwa na TCRA ambapo kanuni 18 zipo chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kanuni 4 zipo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

 

Post a Comment

0 Comments