CHF YAFIKISHA HUDUMA YA BIMA YA AFYA SOKO LA MAJENGO.

 



📌ZAINABU MTOI NA JOSEPHINE MTWEVE                       

MRATIBU wa Mfuko wa Bima ya Afya wa Jamii wa jiji la Dodoma, Patrick Sebigya ametoa wito kwa wafanyabiashara wadogo kujiandikisha kupata huduma ya bima ya afya ili kuhakikisha usalama wa afya zao.

Akizungumza katika banda la wakala wa uelimishaji na uhamasishaji wafanya biashara wa soko la majengo leo jijini Dodoma, Sebigya amesema wameona ni vema kusogeza huduma ya bima karibu na wafanyabiashara wa eneo hilo kusogeza huduma hiyo karibu yao.

Amesema  hawawezi kufanya shughuli zao za kiuchumi ikiwa afya zao zinayumba ila wakishakuwa na bima ya afya wanakuwa na uhakika wa afya zao.

‘’Lengo kubwa ni kuhakikisha kila mwananchi anapata kadi ya bima ili tufikie asilimia 30 ya kaya zilizopo ndani ya jiji la Dodoma,’’ amesema.

Sebigya amesema kwa kutumia njia ya Wakala katika maeneo ya masoko  watawafikia watu wengi zaidi katika jiji la Dodoma

 ‘’Wito wangu kwa wafanyabiashara waliopo hapa waone hii ni fursa ya dhahabu kwamba wasogee hapa waweze kupata huduma za matibabu na awe na amani moyoni,’’ amesema.

Aidha wakala wa uandikishaji wa Shirika la Mfuko wa Bima ya Afya kwa Jamii, Kelvin Sogoe amesema wanakutana na changamoto nyingi kwasababu baadhi ya watanzania  wana mawazo potofu kuhusu uwepo wa wakala katika meneo yao..

Amesema wakati wanaweka kituo hicho baadhi ya watu walikimbia eneo hilo  wakifikiri kwamba ni kampeni ya serikali kujaribu kutoa chanjo ya UVIKO-19.

Sogoe amewasihi wafanyabiashara kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo ili kujiwekea uhakika wa matibabu.

 ‘’Si vema usubiri uanzae kuumwa ndiyo uanze kutafuta bima ya afya,tunatakiwa kujiandaa mapema kabla hatuja shambuliwa na magonjwa’’ amesema.

Vile vile mmoja wa wafanyabiashara wa soko la majengo, Mariam Rugenesi amesema wanaelewa kuwa bima ni muhimu kwa vile gharama za matibabu kwa sasa zipo juu tofauti na kipato cha watu wengi wa hali ya chini.

Amesema anawashauri wafanyabiashara wenzake kukata bima ya afya ilikuepusha gharama za hospitali pale wanapokuwa hawana bima.

 

Post a Comment

0 Comments