DKT. NDUGULILE AKABIDHI RASMI OFISI YA WIZARA KWA DKT. KIJAJI

 

Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi Nyaraka Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji  (kulia) kama ishara ya kumkabidhi rasmi ofisi za Wizara hiyo. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula akishuhudia


MBUNGE wa Kigamboni na aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile leo tarehe 20.09.2021 amekabidhi rasmi Ofisi kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumpa fursa ya kuhudumu katika Wizara hiyo katika kipindi cha miezi sita ya Serikali ya Awamu ya Sita

Aidha, Dkt. Ndugulile ameishukuru Menejimenti ya Wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika kufanya kazi ya kuijenga Wizara hiyo na hatimaye kuongezewa majukumu mengine huku akiyataja baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na Mpango Mkakati wa Wizara, mabadiliko ya Sheria mbalimbali, kuboresha utendaji wa taasisi na kukamilisha muundo wa Wizara

Dkt. Ndugulile amewataka watendaji wa Wizara hiyo kuendeleza mazuri yaliyofanyika na kwa nguvu ileile waendelee kutekeleza mazuri mengi zaidi kwa kushirikiana kwa karibu na Dkt. Kijaji kwa kuwa anaondoka katika Wizara hiyo akiwa ameiacha katika mikono salama



Dkt. Faustine Ndugulile akionesha zawadi ya saa aliyokabidhiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula kwa niaba ya Menejimenti  ya Wizara hiyo kwa kumkumbuka kama kiongozi aliyekuwa akijali muda 


Naye Dkt. Kijaji amemshukuru na kumpongeza Dkt. Faustine Ndugulile kwa kuweka misingi imara katika Wizara hiyo na kufahamika kwa majukumu inayotekeleza kwa kuhakikisha watendaji wa Wizara hiyo na taasisi zake wanashirikiana kwa karibu katika kuwahudumia wananchi

Amesema kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuingia madarakani alimuamini Dkt. Ndugulile kuendelea kuiongoza Wizara hiyo hivyo anapokea Wizara hiyo huku akiamini kuwa kulikuwa na mtu imara aliyetengeneza mazingira mazuri ya kuendelea kutoa huduma bora za Habari, Mawasiliano na TEHAMA kwa wananchi

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) akikabidhiwa zawadi ya saa na Katibu Mkuu wake Dkt. Zainab Chaula kwa niaba ya Menejimenti ya Wizara hiyo kama ishara ya kuonesha kuwa amekuja katika Wizara hiyo kwa wakati sahihi


Aidha, amemtaka Dkt. Ndugulile asifunge milango kwa sababu bado ni mdau mkubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi kupitia utendaji wa Wizara hiyo mtambuka na wezeshi kwa Wizara na taasisi za Serikali katika kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji wa pamoja kupitia huduma za mawasiliano na TEHAMA

Sisi wote ni watanzania lengo letu ni kuijenga Tanzania hivyo uzalendo wetu, upendo wetu pasipo chuki na umoja wetu ndio kitakachofanikisha kutimiza malengo tuliyojiwekea

Dkt. Kijaji

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa amemshukuru Dkt. Ndugulile kwa utumishi wake na kumkaribisha rasmi Waziri wa Wizara mpya ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji na kumuahidi ushirikiano mkubwa katika kuendelea kutimiza majukumu yaliyo mbele yake ya Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo zikiwemo taasisi mbili zilizo chini ya Sekta ya Habari ambazo ni Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa kuna tofauti kubwa iliyoonekana tangu  Wizara hiyo ikiwa Sekta mpaka mabadiliko yaliyoonekana kwa kipindi cha miezi 9 na Menejimenti hiyo imejifunza mengi kupitia kwake ikiwa ni umoja, amani, upendo na mshikamano  na atakaoenda kukutana nao aendelee kuwa zawadi kwao

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Post a Comment

0 Comments