NFRA YANUNUA TANI 4,600 ZA MAHINDI YA WAKULIMA RUKWA

 


📌AMANI KASSIMBA

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) imefanikiwa kununua tani 4,600 za mahindi zenye thamani ya Shilingi Bilioni Mbili na Milioni Mia tatu ( 2,300,000,000) toka kwa wakulima kati ya lengo la tani 5,000 zilizopangwa awamu ya kwanza kufikia Agosti 31, mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo (01.09.2021) wakati Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Milton Lupa alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ofisini kwake Sumbawanga akiwa katika ziara ya kukagua zoezi la ununuzi wa mahindi Meupe linaloendelea katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.



Lupa aliongeza kusema serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuendelea kununua mahindi ya wakulima kulingana na upatikanaji wa fedha.

Wakala unaendelea kufuatilia fedha toka Serikalini ili itekeleze jukumu la kununua mahindi ya wakulima kama ilivyopangwa kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 hivyo wananchi wa Rukwa wawe na subira

Lupa aliongeza kusema Wakala unaendelea kukamilisha ujenzi wa vihenge vya kisasa na kuwa lengo mahindi yote yatakayonunuliwa Rukwa msimu huu yahifadhiwe .



Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alisema wananchi wa Rukwa wamezalisha kwa wingi mahindi kwa kuwa ni zao lao la biashara hivyo wanategemea zaidi NFRA kama soko la uhahika.

Tunaendelea kuiomba serikali itupatie mgao zaidi sisi wana Rukwa kwani zao letu la mahindi ndio zao la biashara kwa wananchi wengi

Kwa mujibu wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya chakula kilimo msimu wa 2020/2021 mkoa wa Rukwa ulizalisha tani 651,433 za mahindi kati ya lengo la tani 731,500 ambapo kutokana na uzalishaji mkubwa mkoa una ziada ya mahindi tani 354,117.

Post a Comment

0 Comments