TAKWIMU: LICHA YA UWEPO WA COVID-19,UCHUMI WAENDELEA KUKUA

 


📌DOTTO KWILASA

LICHA ya kuendelea kuwepo kwa changamoto za UVICO-19,mwenendo wa viashiria vya kiuchumi vya muda mfupi ,Januari -Juni,2021 umeendelea kuimarika kutokana na vichocheo mbalimbali ikiwemo ongezeko la watalii,uzalishaji was saruji ,huduma za mawasiliano na uzalishaji wa Nishati ya umeme

Hayo yameelezwa leo Jijini hapa na Mkurugenzi wa Takwimu za kiuchumi,Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Daniel Masolwa wakati akitolea ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari kuhusu viashiria vinne vyenye mchango kwenye uchumi wa nchi.

Masolwa ameeleza kuwa idadi ya Watalii imeendelea kuongezeka ambapo Kati ya Januari hadi Juni 2021,kiwango Cha Watalii walioingia nchini kiliongezeka kwa asilimia 4.5 ikilinganishwa na kiwango hasi cha asilimia 43.6 kipindi Kama hiki Mwaka 2020.

"Idadi ya Watalii walioingia nchini mwezi Juni 2021 walikuwa 57,689 ikilinganishwa na 9,671 walioingia nchini mwezi Juni 2020,"amesema Masolwa.

Kwa upande wa Uzalishaji wa Saruji nchini  ameeleza kuwa umeendelea kuimarika ambapo ukuaji umeongezeka kwa kiwango hasi cha asilimia 0.6 kutoka kiwango hasi cha asilimia 5.1.

"Pamoja na kwamba huduma nyingi za kiuchumi ziliathiriwa na UVICO-19 ,huduma za Mawasiliano zimeendelea kuongezeka kutoka dakika za kuongea bilioni 31.3 kipindi cha Januari hadi Juni Mwaka 2019 Hadi dakika bilioni 42.9 kipindi Kama hicho Mwaka 2021,"amesema.

Pamoja na hayo ameeleza sababu za kuongezeka Kwa huduma hizonza Mawasiliano keepuwa zimetokana na matumizi makubwa ya huduma wakati wa UVICO-19 kwa kuhusisha uendeshaji wa mikutano Kwa kiwango kikubwa kwa njia ya mtandao.

Licha ya hayo, Mkurugenzi huyo wa Takwimu za kiuchumi ameeleza kuwa uzalishaji wa Nishati ya umeme mwenendo wake umeendelea Kuwa imara ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka saa za kilowatt milioni 3,478 kipindi cha Januari hadi Juni Mwaka 2018 hasi saa za kilowatt milioni 4,053 kipindi Kama hicho Mwaka 2021.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Takwimu za sensa na Takwimu za Jamii Luth Minja amesema Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa Mwaka ulioishia mwezi Agosti,2021 umebaki Kuwa asilimia 3.8 kama ilivyokuwa Kwa Mwaka ulioishia mwezi Julai ,2021 .

Ameeleza kuwa hali hiyo inamaanisha kuwa Kasi ya mabadiliko ya Bei za bidhaa na huduma Kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti ,2021 imekuwa sawa na Kasi iliyokuwepo Kwa mwaka ulioishia mwezi Julai,2021.

 Minja ameeleza pia hali ya Mfumuko wa Bei Kwa baadhi ya nchi za Afrika mashariki Kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti 2021 Kuwa "Nchini Kenya Mfumuko wa Bei umeongezeka Hadi asilimia 6.57 kutoka asilimia 6.55 Kwa mwaka ulioishia mwezi Julai 2021 huku upande wa Uganda umepungua Hadi asilimia 1.9 kutoka asilimia 2.1kwa Mwaka ulioishia mwezi Julai,2021,"amesema.

Kutokana na hayo Mchumi Mkuu kutoka Benki kuu ya Tanzania Stanslaus Mrema amesema kúwa  kazi yao  ni kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa bei kwenye mzunguko wa biashara.

"Tunafanya kazi kutekeleza malengo ambayo Serikali imejiwekea Kwa kuzingatia viwango vya ukuaji wa uchumi,tumepewa jukumu la kusimamia mfumuko wa bei na lengo la kukuza uchumi,"amesema.

Ameeleza kuwa kwa mamlaka waliyopewa ya  utekelezaji wa sera ya fedha Benki kuu huishauri Serikali kuandaa sera zitakazowezesha utulivu wa bei .

 

Post a Comment

0 Comments