TSC YATAKIWA KUTUPIA JICHO UPANDISHAJI MADARAJA WALIMU

 


📌JOSEPHINE MTWEVE

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoan na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Gerald Mweli, ameitaka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kufanya tathimini ya upandishwaji wa madaraja uliokamilika hivi karibuni ili kubaini masuala ya rushwa.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya kamati za walimu kutoka mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida na Manyara jijini Dodoma leo, Mweli  amesema TAMISEMI imepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya walimu  kwamba baadhi ya kamati za walimu katika ngazi za wilaya waliwapandisha madaraja  baadhi ya walimu wasiokuwa na vigezo .

Amesema tathimini inatakiwa ifanyika kwa haraka na kwa uwazi ili waweze kuchukua hatua kwa baadhi ya kamati  za wilaya ambazo zilipandisha walimu madaraja kwa vigezo vya rushwa bila kuzingatia sifa za walimu husika.

Tutakua makini na tutahakikisha haki inatendeka na  hatutoacha kuwasaidia kufanya kazi zenu na kazi mojawapo ni kuwapa mafunzo

Aidha amesema watahakikisha wanaanzisha kituo cha huduma kwa wateja ambapo kitawasaidia walimu muda wowote kupiga simu kuwasilisha malalamiko, maoni na ushauri wao endapo ushauri huo hautafanyiwa kazi   katika ngazi za wilaya.

Naibu katibu huyo amesema Tamisemi imeshaulipa mfumo huo, hivyo tume inatakiwa kuwaandaa wataalamu na chumba maalumu kwaajili ya kupokea malalamiko ya walimu na kuyafanyia kazi.

Mfumo huo unatakiwa kukamilika ndani ya miezi sita na uanze kufanya kazi ili kuwa na taarifa  za ajira, nidhamu na mrejeshomwa rufaa zao

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Profesa Willy Komba aliipongeza Tamisemi  kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu (Elimu) kwa msaada wa kukwamua mambo mbalimbali yakiwemo  ya walimu  kupandisha madaraja.

Profesa Komba amesema anaiomba Tamisemi kuendelea kuwa bega kwa bega na Tume katika kusaidia ajira za walimu, usafiri kwaajili ya walimu wilayani na makao makuu na vifaa pamoja na vitendea kazi vyao.

Naye katibu Mtendaji wa Tume, Paulina Nkwama amesema tume hiyo inaendesha mafunzo kwa kamati za walimu za wilaya kwaajili ya kuwajengea uwezo wa kusaidia masuala ya ajira ya walimu, nidhamu na maendeleo yao.

Amesema wameshafanya mafunzo ya  kujengea uwezo  kamati kanda ya mashariki, kanda ya ziwa na sasa wanafanya katika kanda ya kati , pia anaiomba Tamisemi kuiwezesha kifedha tume ili ikamilishe katika kanda nne zilizobakia.

Post a Comment

0 Comments