WIZARA YA AFYA YASHTUKIA UPOTOSHAJI TAARIFA ZA AFYA MITANDAONI .

 

📌FAUSTINE GIMU

WIZARA ya Afya,Maendeleo ya Jamii,jinsia ,Wazee na Watoto  imetoa onyo na kutahadharisha wanaotoa taarifa ama elimu isiyosahihi na upotoshaji  kuhusu magonjwa yasiyoambukiza .

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 10,2021 jijini Dodoma ,Mganga Mkuu wa Serikali Dkt.Aifello Sichalwe amesema elimu na taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kwa njia ya mitandao ,hasa zikilenga kutoa ushauri wa lishe ,ufanyaji wa mazoezi ,kupunguza uzito ,matibabu ya magonjwa sugu  kama kisukari,saratani  na shinikizo la juu la damu.

Mganga mkuu huyo wa serikali  amesema kwa kuwa watoa elimu hawana sifa  na weledi hali ambayo hupelekea kuleta mkanganyiko katika jamii  kwa kutoa elimu zisizo sahihi.

Napenda kutoa rai kwa Taasisi ,makampuni  na wananchi wenye nia njema ya kusaidia serikali kuelimisha jamii ili kuwezesha kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza  kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa  ni sahihi kwa kuelimisha jamii  kwa kutumia miongozo ya wizara ya afya,kutumia wataalam wenye sifa na weledi katika uelimishaji.

Pia amewataka wadau hao  kuwasiliana na wizara  kupitia kitengo cha mawasiliano serikalini kwa ufafanuzi  na uratibu wa taarifa mbalimbali.

Aidha,Dkt.Sichalwe amesema wizara ya Afya,Maendeleo ya jamii,jinsia,Wazee na Watoto inaendelea kuwakumbusha wananchi wote  kuchukua tahadhari zote za kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza  kwa kufanya mazoezi mara kwa mara  kulingana na ushauri wa wataalam,kupunguza matumizi ya chumvi,sukari na mafuta,kuacha  matumizi ya pombe,kuepuka matumizi ya tumbaku na dawa za kulevya.

Pia,katika kuboresha afya na lishe mganga mkuu huyo wa serikali amewakumbusha wananchi kuzingatia ulaji unaofaa kwa kula mlo kamili kulingana na mazingira yanayowazunguka huku akitoa wito  kwa wananchi wote kufanya uchunguzi wa awali ili kutambua afya zao  na wenye matatizo kuchukua hatua stahiki  za kupata matibabu  kwenye vituo vya kutolea huduma za afya  nchini

 

Post a Comment

0 Comments