WAFANYA BIASHARA WA MTANDAO WATAKIWA KUJISAJILI KATIKA DUKA LA POSTA MTANDAO


 

Na Zena Mohamed, TimesmajiraOnline,Dodoma.

ILI kukuza uchumi na kuondoa utegemezi Shirika la Posta Tanzania (TPC) limewataka wafanyabiashara, wajasiriamali wa mtandao pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kujisajili katika huduma ya duka mtandao (Posta Online shop) lenye zaidi ya lugha 20 zinazotumiwa duniani ili kuongeza wigo wa biashara zao.

Kaimu Posta Masta Mkuu wa TPC  Macrice Mbodo amesema hayo Jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yaliyoambatana na uzinduzi rasmi wa duka la Posta mtandaoni  utakaofanikisha mikakati ya shirika hilo kukuza uchumi na kujitegemea huku akisema duka hilo pia limeenzi lugha ya kiswahili.

Amesema kupitia uzinduzi rasmi wa duka hilo,wamekuja na huduma mpya tatu ambazo ni Posta Kiganjani, Vituo vya Huduma kwa wateja Pamoja na Duka Mtandao. 

Mbodo amesema huduma hiyo inategemea zaidi ushirikiano wa watanzania na kwamba  iwapo Wizara na Taasisi zote zitafungua vituo vya huduma pamoja posta ni wazi huduma nyingi wanazotoa zitapatikana kwa urahisi na kuongeza mapato yatayosaidia kukuza uchumi na kuondoa utegemezi.

"Kupitia huduma ya duka mtandao ambayo inasimamiwa na shirika la Posta Tanzania tumefanikiwa kupata zaidi ya Sh.milioni 300 huku Watanzania wengi wakiendelea kujisajili kutumia huduma hii, juhudi zetu ni kuhakikisha Watanzania wengi wanajiunga na duka mtandao ili kufanya biashara zao kwa gharama ndogo,"anaeleza.

Licha ya hayo Mbodo anasema iwapo Watanzania watatumia shirika hilo ni wazi kuwa thamani ya TPC siku moja itakuwa kama Amazon au Ali Baba kwenye eneo hilo la duka mtandao.

"Tumepiga hatua,kupitia duka mtandao Mteja atajisajili kwa njia ya mtandao, ataweka bidhaa zake na maelezo kama bei, uzito na akishamaliza mteja ataweza kuona bidhaa hizo kupitia duka  mtandao (Posta Online shop)Mteja anaweza kupitia huduma za kifedha za Tigopesa, M-pesa, Airtel Money au kwa Credit Card na Shirika la Posta litaenda kuchukua hiyo bidhaa kwa muuzaji na kuipeleka kwa mteja iwe ndani au nje ya nchi," amesema.

Akielezea dhana inayosambaa kuhusiana na utapeli kwa bidhaa za mtandao, Kaimu huyo amesema Shirika la Posta ni la kiserikali ila itakapotokea kuna hitilafu kwenye bidhaa Shirika litamtafuta muuzaji wa bidhaa ili iweze kubadilishwa na kuipeleka tena kwa mteja, Shirika  hili ni kongwe na limeenea nchi nzima.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Habari , Mawasiliano,Teknolojia na Habari Mhandisi Kundo Methew ametumia nafasi hiyo kueleza Umma historia ya Shirika  la Posta Tanzania (TPC)na kueleza kuwa lilianzishwa mwaka 1994, ambapo hadi sasa linatoa huduma nchini kote na kujinga na mashirika mengine zaidi ya 650,000 duniani.

"TPC inatoa huduma kupokea na kusambaza barua, vifurushi, kadi, magazeti, majarida, huduma ya mtandao, huduma pamoja na nyingine nyingi,dira ya TPC ni kuhutoa huduma ndani na nje katika ubora, kwa wakati na kueleweka,tutahakikisha tunatoa huduma ya bora ambayo inatambulika ulimwenguni na kukidhi malengo ya wateja,"amesema.

Mwisho


Post a Comment

0 Comments