AJIRA UTUMISHI SASA KIGANJANI

 


SEKRETARIETI ya Ajira katika Utumishi wa Umma imezindua App ijulikanayo kama “Ajira Portal Mobile App” ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa waombaji fursa za ajira kupata taarifa za uwepo wa nafasi za kazi, taarifa za nichakato ya ajira kupitia simu zao za kiganjani.

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira  katika Utumishi wa Umma Bw.Xavier Daudi amesema kuwa huduma hii itakuwa inapatikana kwenye Playstore za simu janja na waombaji wa fursa za ajira wataweza kujisajili, kuingia kwenye akaunti zao, kupakia taarifa za vyeti vyao na kuomba kazi kupitia mobile app hiyo.

Aidha,amesema kuwa uwepo wa huduma hii utaongeza wigo wa upashanaji wa habari na kuokoa fedha zilizokuwa zikipelekwa kwenye internet café na baadhi ya waombaji fursa za ajira. Pia amesema mfumo huu utasaidia upatikanaji wa taarifa za walioajiriwa ndani ya sekta ya umma kuwa rahisi zaidi, kuwaondolea usumbufu waombaji wa fursa za ajira kwa kutumia mfumo mmoja wa ajira na utapunguza siku za kuendesha usaili kutoka siku 42 za sasa hadi kufikia siku 38.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mohamed Mchengelwa (Mb) amesema kuwa ili Sekretarieti  ya Ajira iweze kutekeleza kwa ufanishi  majukumu yake inahitaji ushirikiano na uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja katika eneo lake ikiwemo waombaji wa fursa za ajira Serikalini, Waajiri wa Taasisi za Umma na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Nayasema mambo haya ili tuone suala la ajira katika Utumishi wa Umma ni suala la msingi  na muhimu linalotuwezesha kupata nguvu kazi yenye ubunifu,ujuzi na maadili mema ili kuiwezesha Serikali kutekeleza ipasavyo malengo yake inayojiwekea hususani kufikia Uchumi wa kati wa Juu

Hata hivyo  Waziri Mchengelwa ameipongeza  Sekretarieti ya Ajira kwa ubunifu na maboresho ambayo imekuwa ikiyafanya kwa kutumia TEHAMA ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu  yao muhimu.

Waziri Mchengelwa alizindua” Ajira portal Mobile App “jijini Dodoma katika ukumbi wa Tume ya Uchaguzi hafla ambayo ilihudhuriwa na waombaji fursa za ajira katika Utumishi wa Umma, Wawakilishi kutoka  Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta ya Umma  PS3, Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma pamoja na Menejimenti ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Post a Comment

0 Comments