MTAKA:SERIKALI INATAMBUA UMUHIMU WA VYUO VYA UFUNDI

 


📌RHODA SIMBA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthon Mtaka amesema Serikali  inatambua umuhimu wa  vyuo vya ufundi na amewataka vijana wenye fani ya ufundi ujenzi kuchangamkia fursa ya kujenga vyumba vya madarasa jijini hapa  vyenye thamani ya shilingi bilioni 14 .

Aidha fedha hizo  ni zile zilizotolewa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoka benki ya dunia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mpango wa maendeleo ya ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya uviko 19.

Ameyasema hayo jijini hapa katika mahafali ya 36 ya chuo cha ufundi stadi Don bosco kilichopo nje kidogo ya jiji la Dodoma ambapo  pamoja na mambo mengine Mtaka amewatunuku vyeti wahitimu 150 katika ngazi ya cheti na stashahada katika fani mbalimbali.

Mtaka amesema kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa vijana wenye ujuzi mbalimbali ikiwemo ufundi ili waweze kunufaika na fedha hizo  kama Serikali inavyoelekeza hivyo na kuwataka uongozi wa chuo hicho kuwasilisha majina ya wahitimu  ofsini kwake ili waweze kutafutiwa fursa hizo.

"Mpango wa Serikali ni kuhakikisha inajali vijana na hii nchi ina changamoto ya mafundi japo ajira zipo, lakini tatizo linakuja kwa  vijana wenyewe wanapopelekwa kwenye soko la ajira wanaanza kuiba vifaa,na kuonesha tabia zisizofaa mpaka kupelekea kufukuzwa sasa hivi tunajenga vyumba vya madarasa hapa Dodoma vyenye thamani ya shilingi bilioni 14 niwatake mkachangamkie fursa."amesema Mtaka 



Katika hatua nyingine ameutaka uongozi wa chuo hicho kuwa wabunifu ,kuwa na ushindani katika soko la ajira ambapo amewataka kuanzisha kampuni tanzu ya kufanya shughuli mbakimbali kutokana na fani walizonazo ili chuo hicho kiwe kitovu cha kuzalisha malighafi mbalimbali badala ya kuagiza nje ya Mkoa.

"Tunataka Don bosco shindani ambayo itakuwa na Kampuni tanzu ya kufanya shughuli nyingi unakuta mafundi wazuri wanatoka dar  tunataka vijana wakitoka hapa chuoni wawe chachu kwenye Jamii wakienda kwenye Kampuni wanaaminika na kwenda kufanya Kazi kwenye majengo makubwa " 

"Lazima muwe na uso wa kazi mfungue Kampuni zitakazo husiana na fani zenu mnazofundisha  mtapata masoko ,tenda nyingi na kuongeza kipato cha chuo na taifa kwa ujumla huku tukiangalie namna ya kusapoti vijana wenye ujuzi lakini hawana uwezo " amesema Mtaka.

 Kwa upande wake mkuu wa chuo Cha Ufundi Stadi  Don bosco , Padri Boniphace Chami amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1982 kililenga zaidi vijana wasiokuwa na uwezo wa kuendelea na vyuo ambapo walianza na fani nne lakini mpaka sasa imefikia fani 12 ikiwemo fani ya Kilimo.

Aidha amesema kuwa chuo kimekuwa kikiwasaidia vijana kitaaluma kwa kuwatafutia ajira ,kukuza karama michezo,mziki kuwakuza kimalezi na kiimani huku wakipata elimu ya ziada.

"Tumejenga Mahusiano mazuri Kati ya vyuo vya ufundi stadi (VETA),kwa kuwaunganisha wanachuo kupitia soko la ajira, kuzalisha umeme wa solar ambapo tuna kilowatt 34 na kusaidia chuo  kupunguza gharama za umeme,na tumeanzisha fani ya  kilimo ili kuwasaidia vijana wasiwe legelege na kukuza kiwango cha kujitegemea Katika kilimo."amesema Padri Chami



Padri Chami amesema kuwa licha ya mafanikio hayo Bado Kuna changamoto ya mila na desturi mbovu kwa jamii juu mtoto wa kike kusomea fani za ufundi kwa madai kuwa ni kazi ya wanaume na kupelekea wazazi kutowajibika ipasavyo

 Hata hivyo amesema chuo kina mkakati wa kujenga mabweni ya wasichana ambayo watalala hapo ili wapate muda wa kujisomea.

 

 

Post a Comment

0 Comments