SERIKALI YAONGEZA BAJETI KUKABILIANA NA ONGEZEKO LA WANAFUNZI SHULENI

 




Na,Sophia Mohamed, Dodoma.

Kutokana na mafanikio makubwa yaliyoonekana kwenye elimu bila malipo, serikali imeongeza bajeti yake kutoka zaidi ya shilingi Bilioni 21 hadi Bilioni 26 lengo likiwa kukabiliana na ongezeko la wanafunzi shuleni huku zaidi ya bilioni 300 zikitolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa elfu kumi na tano Nchi nzima.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anaeshughulikia elimu, Gerald Mweli wakati akifunga mkutano wa mwaka wa tathmini ya maendeleo ya sekta ya elimu kwa mwaka 2021.

“Tulikuwa tunatoa bilioni 21.8 kuanzia mwezi uliopita tumeanza kutoa bilioni 29.9 tumeongeza kwa sababu kunaongezeko kubwa la watoto”.amesema Mweli

Aidha,ameeleza suala la kuongeza walimu katika vituo vilivyoanzishwa na wananchi ambavyo havipo katika orodha yeyote na kuzifanya kuwa shule kamili kwa sababu vituo vingi watoto walikuwa wakitembea umbali mrefu hadi kufika eneo la shule.

“Vituo vilivyoanzishwa na wananchi ambavyo havipo kwenye orodha tuna mpango wa kuviongezea walimu kwa sababu watoto walikuwa wakitembea kwa kilomita 20 hadi 60, kuanzishwa kwa shule hizi ni jambo zuri hivyo shule hizi tunazifanya ziwe shule kamili.”amesema Mweli

Pia Mweli amezitaka taasisi mbali mbali kuchagua shule zao ili wazijenge na kuziendeleza ili itakapofika mwaka kila mmoja aoneshe angalau shule mbili alizozianzisha.

Kwa upande  wake Majid Mjengwa ambae ni Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO) alieleza  ushirikiano uliopo kati yao na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kupitia  vyuo vya maendeleo ya wananchi ambavyo viko 55 katika usimamizi wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia.

“Tumezungumzia masuala mengi kuhusu elimu ya Tanzania mpango wa mika mitano ijayo ripoti ya mwaka uliopita mafanikio  makubwa yamepatikana  kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kwa kweli Wizara inafanya kazi kubwa.”amesema

Naye Bi.Ignasia Mligo kutoka Chuo kikuu cha Dodoma upande wa elimu idara ya Saikolojia na Mafunzo ya Mtaala ameeleza mambo yaliyozungumzwa katika mkutano wa wadau wa elimu kuwa uwepo wa mikutano kama hiyo ni muhimu kwa kuwa wadau mbalimbali katika sekta ya elimu pamoja na mashirika binafsi hubadilishana mawazo ili kuendelea kuimarisha elimu.

Lengo la Serikali ni kutaka kusaidia watoto kuwa na urahisi wa kupata elimu kwa ufasaha na kwa wakati sahihi.

Post a Comment

0 Comments