IAA YAPONGEZWA KWA MITAALA BORA

 


📌JOSEPHINE MAJURA, WFM, ARUSHA

SERIKALI imeupongeza Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwaandaa wataalam ambao wanakidhi vigezo na matakwa ya soko la ajira Kitaifa na kimataifa kwa kuwa na Mitaala ambayo wanafunzi wanajifunza kwa vitendo zaidi kuliko nadharia.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson wakati wa mahafali ya 23 ya IAA yaliyohusisha wahitimu kutoka Kampasi ya Arusha, Dar es Salaam na Babati yaliyofanyika jijini Arusha.

Nimefurahishwa sana na ongezeko la kozi katika ngazi zote, si ongezeko tu lakini zaidi mitaala yenu inaonesha ni wataalamu wa aina gani mnaozalisha kama Taasisi ya Elimu ya Juu mnatekeleza jukumu lenu la msingi la kutoa elimu kwa viwango ninawapongeza sana

Dkt. Tulia.

Alisema kuwa  orodha ya kozi mnazotoa chuoni nyingi ni zile zinazojibu mahitaji ya wakati kwa kuwa zitatoa mchango mkubwa wa kutoa wataalam watakaosaidia kutatua changamoto mbalimbali katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Dkt. Tulia aliongeza kuwa Serikali inawategemea katika suala la kufanya tafiti zinazoweza kuleta mchango chanya katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kupitia viashiria vya kisekta katika maendeleo ya rasilimali watu, mazingira wezeshi ya biashara, masoko na uratibu na mapinduzi ya kidigitali.



Aidha alitoa rai kwa wahitimu kuhakikisha wanatumia elimu waliyopata kupambana na umaskini kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja, jamii inayomzunguka na Taifa, hatimaye kuisaidia jamii yake kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa letu kwa ujumla.

Ninaamini mtakapotoka hapa baadhi yenu mtaajiriwa  kwenye Taasisi za Umma; wengine mtaajiriwa kwenye sekta binafsi; na wengine mtajiajiri wenyewe kwa kuwa najua mmeandaliwa kufanya kazi katika mazingira yote yaani kuajiriwa na kujiajiri. Nawaomba mkawe waadilifu na mkalitumikie Taifa lenu kwa akili na nguvu zenu zote mkitanguliza uzalendo mbele”, aliongeza Dkt. Tulia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt. Mwamini Tulli, alisema kuwa Chuo kinaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kujua mahitaji ya Watanzania ili kiweze kuanzisha kozi mbalimbali zinazokidhi mahitaji yao ili kuondoa adha wanayoipata Watanzania kwenda kutafuta hizo kozi nje ya Nchi kwa gharama kubwa.

Dkt. Tulli, aliongeza kuwa kozi zinazotolewa Chuo hapo ni kwa ajili ya wazawa na wageni kutoka nje ya Tanzania, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanatimiza vigezo vilivyowekwa kwa kozi husika.

”Nitumie fursa hii pia kuwakaribisha  wazawa  pamoja na wageni toka nchi mbalimbali ambao mmefika hapa hii leo kwa ajili ya kuwashuhudia wapendwa wenu wakitunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali kuja kusoma hapa IAA kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Shahada ya Uzamili. Karibuni Sana IAA”, alisema Dkt. Tulli.

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA),  Prof. Eliamani Sedoyeka, akizungumza wakati wa mahafali ya 23 ya chuo hicho yaliyohusisha wahitimu kutoka Kampasi ya Arusha, Dar es Salaam na Babati yaliyofanyika jijini Arusha.

 

Naye Mkuu wa Chuo Prof. Eliamani Sedoyeka, alisema kuwa kuanzia Januari mwakani Chuo kinatarajia kuanza kutoa Shahada ya Uzamivu yaani Phd kwa kushirikiana na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.

Prof. Sedoyeka aliongeza kuwa Chuo kinatoa takribani kozi 17 kwa ngazi ya Astashahada, kozi 17 ngazi ya Stashahada, kozi 18 ngazi ya Shahada na kozi 12 za Shahada ya Uzamili.

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) ni moja ya kati ya Vyuo sita vilivyopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, jumla ya wanafunzi 2,481 wametunukiwa vyeti katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada ya Uzamili wahitimu.

 

Post a Comment

0 Comments