SERIKALI YARUHUSU USAFIRISHWAJI GUNDI TANI 1683 KWENDA NJE




📌MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ameruhusu kusafirisha jumla ya kontena 93 ya gundi ( utomvu) ambayo sawa na tani 1683 iliyokuwa tayari imeshavunwa wakati akitoa  tamko la kuzuia usafirishaji wa malighafi hiyo  kwenda nchi za nje

Ametoa kauli hiyo leo Jijini Arusha  mara baada ya kupokea ushauri kutoka  kwa  Kamati ya Kumshauri Waziri kuhusu masuala ya misitu kabla ya kufanya mkutano wa Wadau wa mazao ya misitu kuwa gundi hiyo ambayo imekwisha vunwa  inapozidi kukaa inapoteza ubora wake na hivyo kutokufaa tena kwa matumizi tena

Dkt.Ndumbaro amesema amelazimika kuruhusu kusafirishwa kwa tani hizo ili gundi hiyo isiweze kuharibika pamoja na kuepusha hasara ambayo ingewapata   kwa wamiliki pamoja na serikali kukosa mapato kwani Serikali inapata mapato pindi malighafi hiyo inaposafirishwa.

" Hii gundi ni 'Chemicals' inavyozidi kukaa inabadilika rangi na Wataalamu wamenambia kuwa ikiendelea tu kukaa muda wake unaisha wa matumizi " amesisitiza Dkt.Ndumbaro.

Gundi ni aina ya utomvu unaogemwa kwenye miti ya kupandwa aina ya misindano ambapo malighafi hiyo  husafirishwa kwenda nchi za nje lakini hata hivyo  hadi hivi sasa matumizi yake bado hayajaweza kufahamika kuwa inatumikwa kwa ajili ya kutengenezea vitu gani

Hatua hiyo inakuja kufuatia agizo la kusitishwa kuvunwa na kusafirishwa kwa malighafi hiyo kwenda nchi za nje  alilolitoa Dkt. Ndumbaro mwezi Oktoba  akiwa mkoani Iringa mara baada ya kushindwa kupata maelezo ya kutosha kuhusiana na  biashra ya  bei ya gundi hiyo pamoja na matumizi yake huko inakosafirishwa nchi za nje hususani China

Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro ameendelea kushikilia msimamo wake wa kusitisha zoezi la kuvuna utomvu huo hadi pale Chuo cha Kilimo cha Sokoine ( SUA) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania ( TAFORI) zitakapotoa utafiti wake ambao kwa sasa bado haujakamilika juu ya athari ya miti inayovunwa gundi hiyo

Akifafanua katazo hilo Dkt.Ndumbaro amesema katazo hilo lina manufaa makubwa kwa Watanzania kwa ajili ya kutengeza ajira nyingi kwa wananchi

''Mara baada  ya kukamilika kwa ripoti kutoka  TAFORI na  SUA na kujiridhisha kuwa uvunaji hauna madhara wafanyabiashara  mtatakiwa kujenga viwanda hapa nchini na sio habari ya kusafirisha'' amesisitiza Dkt. Ndumbaro

Akizungumzia kuhusiana na Biashara ya Veneer, Dkt. Ndumbaro amewaeleza Wafanyabiashara hao kuwa  yeyote atakayetaka kusafirisha lazima afuate masharti aliyoyato mwezi Noemba akiwa Jijini Dar es Salaam huku akiwata raia wa China wanaofanya biashara hiyo kupitia Chama cha Wafanyabiashara wa China kilichopo nchini kama Wadhamini 

Post a Comment

0 Comments