UKUSANYAJI MAPATO YA NDANI: MANISPAA YA KAHAMA YAONGOZA, MANISPAA YA MOROGORO YAWA YA MWISHO



 ðŸ“ŒOR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba, 2021, Halmashauri zimekusanya jumla ya Sh bilioni 460.2 ambayo ni asilimia 53 ya makisio ya mwaka sawa na asilimia 107 ya lengo la nusu mwaka. 

Waziri Bashungwa amesema makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri katika kipindi cha miezi sita yameongezeka kwa Sh bilioni 78.9 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2020.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo jijini Dodoma hapa wakati wa taarifa za mapato na matumizi ya mapato ya ndani ya halmashauri kati ya Julai hadi Desemba mwaka 2021.

Amesema makusanyo ya halmashauri yaliyoongezeka ni sawa na ongezeko la asilimia 21. Kwa mwaka wa fedha 2021/22, Halmashauri zimepanga kukusanya Sh bilioni 863.9 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani, bajeti hiyo ya imeongezeka kutoka Sh bilioni 814.96 katika mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh bilioni 863.9 katika mwaka wa fedha 2021/22
 

 Katika kipindi hiki Halmashauri za Wilaya za Kishapu na Longido zimeongeza jitihada katika ukusanyaji ukilinganisha na kipindi kama hiki cha mwaka wa fedha 2020/21 ambapo zilikuwa ni Halmashauri za mwisho kwa asilimia ya makusanyo
"Pia zipo baadhi ya Halmashauri ambazo katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka 2021 ufanisi wa kukusanya umeshuka ukilinganisha na kipindi kama hiki cha Julai hadi Desemba mwaka 2020. Moja ya Halmashauri hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ambayo iliongoza kwa asilimia 88 na sasa imeshuka kwa asilimia 20."

Ofisi ya Rais - TAMISEMI ina utaratibu wa kutoa  taarifa ya ukusanyaji wa mapato kila robo mwaka ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri Nchini. Taarifa hii ni ya kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Waziri Bashungwa amesema uchambuzi wa taarifa kuhusu ufanisi wa Halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, unaonyesha kuwa Halmashauri 113 zimekusanya kwa asilimia 50 au zaidi ya lengo la mwaka, na Halmashauri 71 zimekusanya chini ya asilimia 50. 

Hanang yaongoza ukusanyaji wa Mapato ya Ndani

Alisema ulinganisho wa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani unaonyesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imeongoza katika Halmashauri zote 184 kwa kukusanya asilimia 102 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Kaliua, Shinyanga na Mlele ambazo zimekusanya kwa asilimia 91, ya lengo la mwaka.

Hata hivyo, kuna uwezekano wa Halmashauri hizi kuwa na makisio yasiyoakisi uhalisia wa uwezo wake wa ukusanyaji mapato ya ndani hivyo kuhitaji kufanya mapitio ya bajeti ili kuongeza bajeti ya makusanyo na kuweza kuendelea kufanya matumizi ya fedha kutoka kwenye makusanyo hayo
Aidha, Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli na Kilindi zimekuwa za mwisho kwa kukusanya asilimia 27 ikifuatiwa na Halmashauri Wilaya ya Bunda ambayo imekusanya asilimia 28.


 

Jiji la Dar es salaam laongoza kwa wingi wa mapato, Tanga kiasilimia

Waziri Bashungwa akizungumzia kigezo cha wingi wa mapato, amesema  Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam limekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Sh bilioni 36.2 ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyokuwanya Sh bilioni 26.8 na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni  imekusanya Sh bilioni 24.8.
 Aidha, Halmashauri 13 kati ya 184 zimekusanya kuanzia Sh bilioni 5 na zaidi.

Bashungwa amesema Mkoa wa Manyara umeongoza kwa kukusanya asilimia 69 ya lengo la mwaka, ikifuatiwa na Mkoa wa Songwe asilimia 68, Mkoa wa Njombe asilimia 64 na Ruvuma asilimia 61 huku Kilimanjaro ikiwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 43 ukifuatiwa na Mkoa wa Kigoma asilimia 44 na Mkoa wa Mara asilimia 45.

Makusanyo kwa Halmashauri za Majiji, Bashungwa alisema Jiji la Tanga limeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 56 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Jiji la Arusha  ambalo limekusanya kwa asilimia 55 na Jiji la Mwanza kwa asilimia 54. 

Amesema Jiji la Mbeya limekuwa la mwisho kwa kukusanya mapato kwa asilimia 45 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Jiji la Dar es Salaam kwa asilimia 52 na Jiji la Dodoma kwa asilimia 53.

Manispaa ya Kahama yaongoza, Manispaa ya Morogoro yawa ya mwisho, Ukusanyaji wa Mapato ya ndani

Kwa upande wa Halmashauri za Manispaa, Bashungwa alisema Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 67 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kwa asilimia 65 na Manispaa ya Ilemela kwa asilimia 55. 

Katika kundi hili Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya asilimia 37 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri za Manispaa ya Kigoma asilimia 38 na Ubungo asilimia 40.

Kwa upande wa Halmashauri za Miji, Bashungwa amesema Halmashauri ya Mji wa Mbulu imeongoza kwa kukusanya asilimia 83 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri za Miji ya Tunduma kwa asilimia 79 na Njombe kwa asilimia 73. 

Waziri Bashungwa amesema Halmashauri ya Mji wa Korogwe imekuwa ya mwisho kwa kukusanya kwa asilimia 39 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji ya Nzega kwa asilimia 42 na Halmashauri ya Mji Masasi kwa asilimia 42.

Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imeongoza kwa kukusanya asilimia 102 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Kaliua, Shinyanga na Mlele ambazo zimekusanya kwa asilimia 91.  

Aidha, Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli na Kilindi zimekua za mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 27 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambayo imekusanya kwa asilimia 28 ya makisio ya mwaka

Bil. 128 za mapato ya ndani zatumika kwenye Miradi ya maendeleo

Bashungwa amesema uchambuzi unaonesha kuwa Halmashauri zimetumia Sh bilioni 129.1 sawa na asilimia 76 ya fedha zilizopaswa kutumika kwenye miradi ya maendeleo ambazo ni Sh bilioni 170.4 ya mapato yasiyolindwa Sh bilioni 356.7 ya mapato yaliyokusanywa kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2021.

  Amesema halmashauri 31 zimetumia asilimia 100 au zaidi ya kiasi kilichopaswa kutumika, Halmashauri 128 zimetumia kati ya asilimia 50 na 99 ya kiasi kilichopaswa kutumika, Halmashauri 25 zimetumia chini ya asilimia 50 ya kiasi kilichopaswa kutumika.

 Aidha, taarifa zinaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji imeongoza kwa kuchangia asilimia 148 ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya  Ngorongoro kwa asilimia 146 na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kwa asilimia 142 .
Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma imekuwa ya mwisho kwa kuchangia asilimia 18 ikifuatiwa na Halmashauri ya Bumbuli kwa asilimia 20, na Halmashauri ya Mji ya Mafinga kwa asilimia 26.

Post a Comment

0 Comments