DKT. GWAJIMA ATAKA WADAU WOTE KUINGIA MAPAMBANO YA UKEKETAJI KWA WANAWAKE NA WATOTO


📌 MJJWM

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema vita dhidi ya  ukatili ukiwemo Ukeketaji nchini, inatakiwa kuhusisha watu wa kada zote ili muleta mafanikio yaliyokusudiwa.

Waziri Dkt. Gwajima, ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na wandishi wa Habari ikiwa ni kuelekea kilele cha Siku ya kupinga Ukeketaji inayoadhimishwa katika ngazi ya mikoa hasa yenye viwango vya Juu vya  Ukeketaji.

 Kaulimbiu ya Siku ya Kupinga Ukeketaji kwa mwaka 2022  ni “Tuongeze Uwekezaji, Kutokomeza Ukeketaji” ambayo inahimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwa pamoja na Tanzania kuongeza uwekezaji wa rasilimali za kutosha ili kutekeleza afua za kuzuia na kukabiliana na athari za ukeketaji ikiwa pamoja na kuwabaini na kuwasaidia wahanga wa ukeketaji katika jamii.

“Hali ya ukeketaji imekuwa inapungua mwaka hadi mwaka kunatokana na jitihada za Serikali, asasi za kiraia na wadau wengine wanaoshiriki katika kutokomeza ukeketaji na kubadili mitizamo ya jamii kuhusu mwanamke na mtoto wa kike”, alisema Waziri Dkt. Gwajima. 

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa hali ya ukeketaji imepungua kutoka asilimia 18 mwaka 1996 kufikia asilimia 15 mwaka 2010 na asilimia 10 mwaka 2015/16, aidha kupungua huku bado jitihada zaidi zinahitajika hususan kwa  Mikoa yenye hali ya juu ambayo ni  Manyara  yenye asilimia 58, Dodoma asilimia 47, Arusha asilimia 41,  Mara wenye asilimia 32 pamoja na Singida ambayo ina asilimia 31. 

Waziri Gwajima, ameitaka jamii ikiwepo kundi la wanahabari kupaza sauti zao  kwa pamoja katika vita hiyo, kwakutumia vyombo vyao vya Habari bila yakupotosha kwakushirikiana na jamii na kuibua changamoto zilizopo na kuja na majibu ya pamoja yatakayo inusuru jamii na madhila ya uekeketaji.Wadau wote wakiwepo wanahabari tuweke mikakati ya pamoja ya kuifikia na kuelimisha jamii katika kufikia malengo yakupunguza kutoka asilimia 8 iliyopo kwasasa hadi asilimia 5
Waziri Dkt. Gwajima

Dkt. Gwajima amesema, Serikali katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini  kwa kushirikiana na wadau wamefanikiwa kuanzishwa kwa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 18,618 kwenye Mikoa, Halmashauri, Kata hadi ngazi za Vijiji/Mtaa mbalimbali. 

Aidha, nyumba salama 9 zimeanzishwa kwa ajili ya kuwahifadhi na kuwatunza waathirika waliokimbia ukeketaji kwenye mikoa yenye kiwango cha juu cha ukeketaji, jitihada zingine ni kuanzishwa kwa vituo vya mkono kwa mkono 14 kwenye Mikoa 10 ya Tanzania Bara, sambamba na kuanzishwa kwa Dawati la Jinsia na Watoto katika vituo 420 vya Jeshi la Polisi nchini.

Waziri Dkt. Gwajima, amefafanua kuwa Serikali pia imetunga na kuzifanyia maboresho Sheria mbalimbali ili kuimarisha ulinzi wa wanawake na watoto nchini kutokana na vitendo vya ukatili ikiwemo Ukeketaji

“Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 ya mwaka 2002, kifungu cha 158 (1) (a) na Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 ambayo inazuia ukeketaji kwa mtoto wa kike. Aidha,  Serikali imeandaa na inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji wa 2021/22 – 2024/25” amefafanua Waziri Dkt. Gwajima.

Post a Comment

0 Comments