MFUMUKO WA BEI WAPUNGUA: KODI YA PANGO,NYUMBA ZA KULALA WAGENI ZASHUKA

 


📌RHODA SIMBA

MFUMUKO  wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Januari ,2022  umepungua hadi asilimia 4.0% kutoka asilimia 4.2% kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2021 .

Hayo yamesemwa leo Februari 8,2022 jijini hapa na Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya watu na takwimu za jamii  kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Ruth Minja wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema  hii ikimaanisha kuwa ,kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Januari ,2022 imepungua ikilinganishwa  na kasi iliyokuwepo  kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba,2021.

Amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Mwezi Januari ,2022   kumechangiwa hasa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa  zisizo za vyakula  kwa kipindi kilichoishia mwezi Januari ,2022  ikilinganishwa na kipindi kilichoishia mwezi  Disemba 2021 .

“Mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi  kwa mwezi Januari ,2022  umepungua kwa asilimia 3.1%  kutoka asilimia 3.9% kwa ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2021 huku mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula visivyochakatwa ,nishati na bili za maji [Core Inflation] kwa mwezi Januari  2022  umepungua hadi asilimia 3.3% kutoka asilimia 4.6%  ilivyokuwa mwezi Disemba 2021”amesema Minja

SOMA HII PIA:WAZIRI UMMY AWATAKA WANAUME KUACHA UOGA VIPIMO VYATEZI DUME

Aidha ,kaimu Mkurugenzi huyo ameainisha baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula  zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na mavazi  kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 2.8%,viatu kutoka asilimia 4.6% hadi asilimia 4.4%,kodi ya pango  kutoka asilimia  4.4%  asilimia 1.2%.magodoro kutoka asilimia 12.3%hadi asilimia 7.3%,majokofu kutoka asilimia 4.2 hadi asilimia 1.5%,cherehani kutoka asilimia 9.1% hadi asilimia 5.0%, simu janja kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 3.3%.

Vingine ni vyombo vya nyumbani kama sahani kutoka asilimia  kutoka asilimia 16.7%  hadi asilimia 3.6% ,luninga kutoka asilimia 3.5% hadi asilimia 1.2% na malazi kwenye hoteli  na nyumba za kulala wageni kutoka asilimia  kutoka asilimia 6.6%  hadi asilimia 2.9%

Katika hatua nyingine Bi.Minja ameainisha mfumuko wa bei   kwa nchi za Afrika Mashariki  ambapo nchini Uganda  umepungua hadi asilimia 2.7% kutoka asilimia 2.9 % huku nchini Kenya  ukipungua pia kutoka asilimia 5.39 % kutoka asilimia  5.73.

 

 

Post a Comment

0 Comments