LGTI KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA KWA KUTOA HUDUMA BORA ZINAZO IMARISHA UTAWALA BORA.

 

📌DOTTO KWILASA 

KATIKA kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo-Dodoma (LGTI) kimetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.8 kujenga madarasa mapya, nyumba za watumishi, jengo la utawala na Cumpus ya Dodoma ili kuwezesha huduma bora zitakazo wajengea wananchi uwezo wa kuimarisha utawala bora.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Chuo hicho Dkt.Mpamila Madale wakati akiongea na Waandishi wa habari chuoni hapo kuhusu mafanikio yaliyopatikana LGTI ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia na kueleza lengo la kufanya hivyo ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya elimu huku tukijipanga kutoa wahitimu ambao watakuwa na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa.

 Amefafanua kuwa Shilingi milioni 550 ni kwa ajili ya kukarabati nyumba za wafanyakazi, mabweni na maktaba wakati Shilingi milioni 907 ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala kwa awamu ya kwanza ambalo litagharimu bilioni 4 hadi kukamilika kwake,Mil 350 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, Shilingi milioni 255 Kwa ujenzi wa Cumpus ya Dodoma mjini utakaogharimu bilioni 14 mpaka kukamilika kwake.

Kwa kutambua umuhimu wa kuwafikia walengwa wa elimu,Serikali ya awamu ya sita imetupatia eneo lililokuwa Ofisi ya zamani ya mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili kujenga kampasi kubwa ya kisasa,LGTI tunamshukuru sana,na niseme wazi kuwa tuna imani naye na tutashirikiana naye bega kwa bega kufanikisha lengo la Serikali katika kutoa huduma bora 

Mkuu huyo wa LGTI ametaja pia mafanikio mengine ambayo yamepatikana katika kipindi cha awamu ya sita chuoni hapo kuwa ni pamoja na kutunza mazingira kwa kupanda miti zaidi ya 1000 hali inayo saidia kuweka mandhari safi na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Katika masuala ya uhifadhi.

Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo hicho, Taaluma,Utafiti na Ushauri, Dkt.Michael Msendekwa amesema wamejipanga kuendelea kutoa elimu yenye ubora ikiwa ni pamoja na kuiweka sawa mitaala ambayo itawafanya wanafunzi watoke wakiwa na uwezo wa kujiari na kuajiriwa.

Dkt.Msendekwa amesema wameongeza baadhi ya kozi pamoja na kuwapeleka wafanyakazi kwenda kusoma zaidi ili kuongeza ubora wa elimu katika chuo hicho.

Chuo kimejipanga kukabiliana na changamoto ya ukatili wa kijinsia ambao umeendelea kujitokeza katika jamii kwa kuongeza baadhi ya kozi ambazo zitasaidia kulinda mmonyoko wa maadili

Kuhusiana na mafaniko mengine Naibu Mkuu wa Chuo hicho ,Mipango,Fedha na Utawala,Mashala Yusuph ameyataja mafanikio mengine ni kuongeza idadi ya watumishi kutoka 203 hadi 216 kwa mchanganuo wa wanaume 83 na wanawake 133.

Ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia, chuo kimewapeleka masomoni watumishi 44 kati yao 21 wanasoma shahada ya uzamivu,10 wanasoma shahada ya uzamili na 13 wanasoma shahada ya kwanza na wengine 8 wamemaliza na kuripoti kazini kati ya hao 2 wamehitimu shahada ya uzamivu,4 shahada ya uzamili na 2 shahada ya kwanza

 Mwishoo.

 

Post a Comment

0 Comments