MTAKA AITAKA TFS KUONGEZA JITIHADA ZA UPANDAJI NA UTUNZAJI MITI CHANZO CHA MAJI MZAKWE

 



📌RHODA SIMBA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ameitaka wakala wa Misitu Tanzania (TFS) pamoja na uongozi wa bonde la maji la Wami Ruvu kuongeza jitihada za upandaji na utunzaji wa miti katika chanzo cha maji Mzakwe mkoani Dodoma.

Mtaka amebainisha hayo jijini hapa mara baada ya kutembelea katika eneo la upandaji wa miti katika chanzo hicho cha maji ambacho ni chanzo muhimu cha maji mkoani Dodoma na kutoridhishwa na hali ya upandaji wa miti katika eneo hilo lenye zaidi ekari elfu nne, ikiwa ni sehemu ya ziara yake maalum kuhusu masuala ya utunzaji wa mazingira.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amesema takwimu zinazotolewa juu ya idadi ya miti iliyopandwa katika eneo hilo haziendani na hali halisi na kuwataka viongozi wa bonde kuacha uzembe  na kudanganya viongozi wakuu wa nchi.

Kutokana na baadhi ya jamii inayozunguka katika chanzo cha maji Mzakwe kuwa na tabia ya kuingiza mifugo pamoja na kuchoma moto chanzo hicho, mkuu huyo wa mkoa ameagiza sheria zitekelezwe ikiwemo faini ya kuanzia Tsh. Elfu hamsini (50,000/=) hadi Tsh laki tatu (300,000/=)

Katibu tawala mkoa wa Dodoma Dkt.Fatuma Mganga amesema kuna umuhimu wa uratibu mzuri wa utunzaji wa miti katika chanzo hicho, huku Mstahiki Meya jiji la Dodoma Prof.Davis Mwamfupe akizungumzia umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii ya eneo husika katika utunzaji wa chanzo hicho ambapo mkazi wa Makutupora mtaa unaozunguka eneo la hifadhi ya chanzo cha maji Mzakwe Mzee Shaban Nyambo akishauri aina ya miti ya asili inayopaswa na kustahimili eneo hilo kuwa ni pamoja na migunga na mikambala.


                                

                                  

Mhifadhi misitu na wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kanda ya kati Alexanda Mboya ameanisha changamoto zilizosababisha miti iliyopandwa kutostawi katika eneo hilo kuwa ni pamoja na mbuga hivyo mahitaji ya eneo hilo la chanzo cha maji Mzakwe ni miti ya asili huku Mkuu wa kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makutupora Resto Mbanga akisema kuna uhitaji wa ushirikiano wa kulinda eneo hilo.





Post a Comment

0 Comments