SINGIDA WAIOMBA SERIKALI KUONGEZA BAJETI ELIMU

 


📌RACHEL CHIBWETE


WAKAZI wa Mkoa wa Singida wameiomba serikali ya mkoa huo kuongeza bajeti ya elimu ili iweze kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu Mkoani humo.

Wakizungumza Jijini Dodoma kwenye kikao cha kupokea ripoti ya  mianya ya mapato ya kodi iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la ActionAid baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya wamesema bado kuna changamoto nyingi kwenye sekta ya elimu kwenye halmashauri hiyo.

Faudhia Said mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, amesema sekta ya elimu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Singida bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na madawati hali inayosababisha wanafunzi kujifunza kwenye mazingira magumu.

Amesema ili kutatua changamoto za elimu kwenye Halmashauri hiyo  ni lazima Halmashauri hiyo itenge asilimia 20 ya bajeti kuu kwa ajili ya elimu kwani mpaka sasa hivi Halmashauri ya Wilaya ya Singida haijafikia asilimia hiyo.

Amesema sekta ya elimu ina changamoto nyingi ambazo kama hazitatengewa pesa ya kutosha kwenye bajeti changamoto hizo hazitaweza kutatuliwa.


 

Kwa upande wake Maria Stephen amesema ili kutatua changamoto kwenye sekta ya elimu inabidi fedha za mfuko wa Jimbo zitumike kutatua changamoto hizo kwa awamu 

"Jimbo la Singida lenye Tarafa 3 zenye jumla ya  kata 21 linapata pesa za mfuko wa Jimbo  milioni 61.2/- kila mwaka, hivyo kama fedha hizo zitapelekwa kutatua changamoto za elimu zitasaidia sana kwenye ujenzi wa vyoo, madarasa na hata nyumba za walimu," amesema Maria.

Ameongeza kuwa, "Lakini fedha za mfuko wa Jimbo zinaonekana hazina faida yoyote kwa jamii kwa sababu zinagawanywa kidogo kidogo kwenye Jimbo lote lakini kama zingetengewa kipaumbele cha kukamilisha miradi hasa ya elimu zingeonekana zinafanya kazi tofauti na ilivyo hivi sasa.''

Naye Yasin Lila ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Singida kuanzisha vyanzo vingine vya mapato ili kuongeza ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashauri hiyo ili inapopanga bajeti zake ziweze kutimizwa kwa kiasi kikubwa.

"Kuna maeneo ambayo yanatoa madini mbalimbali kama vile mchanga, kokoto na mawe usimamizi kwenye maeneo hayo inabidi uongezwe ili mapato yapatikane, pia kuna masoko ambayo yamejengwa lakini hayatumiki masoko hayo yakafunguliwe ili Halmashauri ipate mapato yake," amesema Lila.

Akizungumza kwenye kikao hicho mwakilishi wa Katibu tawala wa mkoa wa Singida, ambaye ni Afisa Elimu wa mkoa huo, Mary Lyimo amesema kuwa serikali inajitahidi kumaliza changamoto kwenye sekta ya elimu kwani kwa kutumia fedha za Uviko 19 mkoa huo umetumia Sh 30.7 Bilion kwenye sekta ya elimu pekee.

Amesema fedha hizo zimepunguza changamoto mbalimbali kwenye sekta ya elimu kwani zimetumika kujenga vyumba vya madarasa, ujenzi wa vyoo, madawati na nyumba za walimu kwenye Halmashauri zote za mkoa wa Singida.

Lyimo amesema pia kuna wafadhili mbalimbali ambao wamekuwa wakifadhili masuala ya elimu na kuwataka wananchi wa Halmashauri zote za mkoa wa Singida kujitokeza na kujitolea kwenye shughuli zinazohusu elimu badala ya kuiachia Serikali peke yake

Akitoa taarifa ya ripoti ya mianya ya kodi  ambayo inaisababishia serikali upotevu mkubwa wa mapato, Mshauri wa masuala ya kodi kutoka shirika la Action Aid, Dk Balozi Morwa amesema kuna mianya mingi ya kodi ambayo inaisababishia serikali upotevu mkubwa wa mapato.

Amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2021 serikali imepoteza kiasi cha trilioni 17/- kutokana na mianya mbalimbali ya rushwa ikiwemo misamaha ya kodi kwa wawekezaji wapya.

Dk Morwa amesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa ambapo kingeweza kumaliza baadhi ya changamoto kwenye sekta ya elimu na fedha nyingine zingebaki kwa ajili ya kufanyia shughuli nyingine za kimaendeleo.

Amesema Serikali idhibiti mianya hiyo ya upotevu wa mapato ambapo mapato mengi yanapotea kupitia, sekta isiyo rasmi, utakatishaji wa fedha, kesi za mapato zilizoko mahakamani, misamaha ya kodi, mikataba ya wawezaji ambayo ina masharti ya kutotoza kodi kwa bidhaa zisizozalishwa nchini, ukusanyaji wa mapato kupitia mashine za kieletroniki na mikataba ya wafanya biashara wanaolipa kodi kidogo kidogo.

 

Post a Comment

0 Comments