📌RHODA SIMBA
IMEBAINISHWA kuwa wakina mama 30 wanakufa kila siku,na wengine elfu 11,000 wanakufa kwa mwaka, sababu kubwa za vifo hivyo vikitajwa kuwa ni kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Kadhalika Utoaji mimba usio salama umetajwa kwa (asilimia 19), Kifafa cha mimba (asilimia 17), uzazi pingamizi (asilima 11) na uambukizo (asilimia 11), huku sababu nyingine zinazochangia ni pamoja na ukosefu wa damu, malaria na maambukizi ya Virus Vya UKIMWI.
Akizungumza jijini Dodoma katika kilele cha siku ya wakunga duniani Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Switbert Mkama amesema kuwa pamoja na kuwa na ongezeko la akina mama kuhudhuria kiliniki na kujifungulia katika vituo vya huduma lakini takwimu zimeonesha ongezeko la vifo vya wanawake wajawazito kutoka 454 hadi kufikia vifo 556 kwa kila vizazi hai laki 100,000.
"Nimeelezwa kuwa jumla ya wanawake wajawazito 2,373,668 waliohudhuria kiliniki 1,636,273 ( asilimia 69) walipimwa wingi wa damu, 1858856 ( asilimia 71 ) walipata chanjo ya kuzuia pepopunda,
Waliojifungulia katika vituo vya huduma walikuwa 1778987, kati ya hao walizalishwa na Wakunga watalaam walikuwa 1657170 ( (asilimia 93 ),"amesema.
Kwa hizi takwimu chache zinadhihirisha kazi kubwa inayofanywa na wakunga katika kutoa huduma kwa wanawake wajawazito na watoto.
"Kwa mfano asilimia ya wajawazito wanaohudhuria kliniki imeongezeka na kufikia asilimia 98, idadi ya wakina mama wanaojifungulia katika vituo vya huduma kutoka asilimia 47 hadi asilima 63,"amefafanua.
Aidha alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 81 hadi 67 kwa kila vizazi hai 1000.
Amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa na jitihada za wakunga kwani hata mafanikio yaliyopo katika kupunguza vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja na watoto chini ya miaka mitano inatokana na kazi nzuri wanazozifanya wakunga hapa nchini.
Pia amesema kuwa shahidi kutoka tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa mkunga akielimishwa na kufikia kiwango cha kimataifa kulingana na Shirikisho la Vyama vya Wakunga Duniani anaweza kutoa huduma za kuokoa maisha kwa mama na mtoto mchanga kwa asilimia 87.
Kwa upande wake rais wa Chama Cha Wakunga Tanzania Bi Feddy Mwanga alisema kuwa wakunga 200 waliotoka sehemu mbalimbali nchini waliweza kuhudhuria katika Kongamano hilo.
Amesema Kongamano hilo lilikuwa na mafanikio makubwa kwani wakunga na wadau wa Afya ya mama na mtoto walijitoa katika kuleta abstracts na kutoa mada ambazo zilikuwa za kuelimisha na kutoa matokeo ya tafiti mbalimbali.
Pia amesema waliweza kubadilishana uzoefu au kupeana taarifa mpya na mabadiliko kadhaa yaliyotokea kwenye taaluma ya ukinga.
"Kama ulivyoona wakunga na wadau walionyesha shughuli mbalimbali za ukinga katika mabanda uliyotembelea kumekuwa pia na vipindi vya kujengeana uwezo kwa kufundisha Jinsi ya kuhudumia wakinamama na watoto wachanga,"amesema.
Napenda nitambue na kuwashukuru sana mashirika ya umoja wa
mataifa yakiongozwa na UNFPA ambapo tumekuwa nao katika safari nzima ya
maandalizi ya shughuli hii pamoja na mashirika mengine.
Siku ya Wakunga huadhimishwa duniani kote tarehe tano mwezi wa tano ya kila
mwaka kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na Wakunga pamoja na
kuwahamasisha Wadau mbalimbali na Jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa
huduma bora kwa akina mama na watoto.
Kauli Mbiu ya Mwaka huu ni “Invest in Midwives: Save lives ” kwa maana ya “Wekeza kwa Mkunga: Okoa Maisha”.
0 Comments