WAZIRI MKUU KUZINDUA MPANGO WA KITAIFA WA UHIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

 

📌RHODA SIMBA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira  Dk Selemani Jafo ametoa Tamko la Siku ya Mazingira Duniani leo Mei 27, 2022 jijini Dodoma ambapo amesema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua Mpango wa Kitaifa wa Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira katika kilele cha Siku ya Mazingira Duniani Juni 5, 2022.

Waziri Mkuu atamwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango.

Pia mpango huo umebainisha changamoto za mazingira kuanzia ngazi ya mamlaka za Serikali za Mitaa, Mikoa pamoja na mifumo-ikolojia mahususi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo Mei 27 jijini hapa Dkt.Selemani Jafo amesema kuwa mpango kabambe huo umetoa mapendekezo ya hatua za kukabiliana na changamoto husika kuendana na mahitaji ya kila eneo.

‘’Kwa muktadha huo, mpango kabambe wa hifadhi na usimamizi wa Mazingira utakuwa  ndio nyenzo muhimu katika kutoa muongozo wa kuandaa na kutekeleza miradi na programu za kuhifadhi mazingira nchini,’’amesema Dkt.Jafo. 

Aidha amesema kuwa  imeeleza kuwa takriban kiasi cha hekta 469,420 za misitu huharibiwa kila mwaka kwa utupaji holela wa taka pamoja na  uwepo wa athari za mabadiliko ya tabianchi yamekuwa ni changamoto kubwa katika nchi hali hiyo inaathiri maisha ya viumbe mbalimbali ikiwemo ya mifumo ikolojia ambapo  hadi sasa imeliletea Taifa hasara ya  takriban asilimia tano (5%) ya Pato la Taifa.

Amesema kuwa inafahamika  kwamba nchi  inakabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira  ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji, uharibifu wa Makazi ya wanyamapori na Bioanuai hali hiyo  inasababishwa na matumizi yasiyo endelevu yanayochochewa  na utegemezi mkubwa wa jamii kwenye maliasili.

Kutokana na hali hii, Hivyo maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaendelee kuwa chachu ya  kuongeza  kasi ya uhamasishaji  wa jamii  kushiriki shughuli za kuhifadhi na kutunza mazingira nchini

Aidha amezishauri Halmashauri za Mikoa yote kuhamasishana na kuelimisha jamii masuala yahusuyo hifadhi ya mazingira ikiwemo kutumia nishati mbadala wa mkaa majiko banifu pamoja na kutumia njia sahihi za kuhifadhi taka  kwamba, suala  la hifadhi ya mazingira ni jukumu lakila mtu  na linapaswa kutekelezwa kwa vitendo.

“Natoa wito kwa watanzania wote kufahamu kuwa utunzaji na uhifadhi wa mazingira ni jukumu letu sote,kila mmoja kwa nafasi yake kwakuwa tusipotunza mazingira yetu sisi wenyewe, hakuna mtu yoyote kutoka kwingine atatufanyia kazi hiyo na hiyo kupelekea nchi yetu kukumbwa na majanga makubwa kama vile ukame, mafuriko, ukosefu wa chakula, upungufu wa maji”amesema Jafo

 Pia hata ukosefu wa amani na utulivu nchini kutokana na upungufu wa rasilimali muhimu zinazowezesha maisha yetu, Napenda kuwakumbusha kuwa mazingira ya nchi yetu yakiharibika hatutakuwa na pahala kwingine pa kwenda kuishi kwa furaha na amani zaidi ya Tanzania yetu

 Dkt.Jafo. 

Aidha amesema kuwa Maadhimisho ya Kitaifa mwaka huu yatafanyika hapa Jijini  Dodoma na kaulimbiu ya kitaifa  inayoongoza maadhimisho haya ni Tanzania ni moja tu: Tutunze Mazingira  Hali kadhalika, kaulimbiu hii inatuhamasisha sisi wana nchi kwa pamoja kila mmoja katika shughuli zake za kila siku kutunza mazingira ya nchi yetu ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa mahali salama pa kuishi kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

“Kilele cha maadhimisho haya kitatanguliwa na Wiki ya Mazingira inayoanza tarehe 28 Mei  4 Juni 2022,Katika Wiki shughuli mbalimbali za hifadhi na usafi wa mazingira zitafanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma zikuhusisha wananchi, taasisi, mashule, vyuo na viongozi mbalimbali,”alisema Dkt.Jafo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dk.Andrew Komba alisema kuwa bado baadhi ya watu wanachafua Mazingira kwa makusudi nakusababisha magonjwa ya mlipuko naya kuambukizwa ikiwa ni pamoja na kuhara ,kipindupindu, kutapika na yake yanayitokana na Mazingira machafu.



Hata hivyo Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kimataifa mwaka huu  ni Only One Earth, ambayo kwa tafsiri ya lugha ya kiswahili isiyo rasmi ni Dunia ni moja Tu kaulimbiu hii inatanabaisha jumuiya ya kimatafa kuwa Dunia ambayo ndio nyumba yetu wote, ni moja tu na hakuna mbadala wake.

 


Post a Comment

0 Comments