BILIONI 889.2 ZATENGWA UJEZI WA SKIMU ZA MAJI VIJIJINI

 


📌JASMINE SHAMWEPU

SERIKALI imetenga jumla ya shilingi Bilioni 889.2 kwa ajili ya ujenzi wa skimu za maji vijijni kupitia wakala wa maji vijijini na usafi wa Mazingira RUWASA kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wake, utekelezaji, mwelekeo na mafanikio ya RUWASA.

Amesema kuundwa kwa RUWASA ulikuwa ni uamuzi sahihi na makini uliofanywa na Serikali katika jitihada zake za kuwapatia wananchi huduma muhimu za kijamii.

Amesema RUWASA inatekeleza shughuli zake kwa kuongozwa na Mpango mkakati wa miaka mitano, yaani 2020/2021 hadi 2024/2025.

 Pamoja na hatua hiyo ya kuundwa kwa RUWASA, Serikali imeongeza uwezeshaji wa rasilimali fedha ili kuongeza kasi ya kuwapatia wananchi waishio vijijini huduma endelevu ya maji safi na salama

Mwaka wa fedha 2022/23 Wakala wa Maji Vjijini (RUWASA) umepanga kutekeleza jumla ya miradi 1,029 huku kati ya miradi hiyo 381 ni mipya na miradi 648 ikiwa ni ile ambayo utekelezaji wake unaendelea kutoka mwaka wa fedha uliopita

Kivegalo .

Aidha amesema kukamilika kwa miradi hiyo, kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kuongezeka kwa wastani wa asilimia sita na kwamba utekelezaji wa shughuli zake unaongozwa na Mpango Mkakati wa miaka mitano, yaani 2020/2021 hadi 2024/2025 utakaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini hadi kufikia kiwango kisichopungua asilimia 85 kwa mwaka 2025.

Akieleza hali ya upatikanaji wa maji kabla na baada ya kuundwa RUWASA, Mhandisi Kivegalo amesema, wakati wa kuanzishwa kwake, RUWASA ilirithi jumla ya skimu za maji 1,379 zilizokuwa zimekamilika na kulikuwa na miradi 632 ya ujenzi wa skimu za usambazaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini na kueleza kuwa kati ya skimu hizo zilizokuwa zimekamilika 177 zilikuwa hazitoi huduma ya maji kwa wananchi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukauka kwa vyanzo vya maji.

Amefafanua kuwa mwezi Julai 2019 upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ulikuwa ni wastani wa asilimia 64.8 ambapo pamoja na kiwango hicho cha upatikanaji wa maji, kwa ujumla, hali ya huduma ya maji vijijini haikuwa ya kuridhisha. 

Sambamba na hayo alisema ujenzi wa miradi ulikuwa ukichukua muda mrefu na kwamba hata miradi iliyokuwa ikikamilika na kuzinduliwa, ilidumu muda mfupi na kusababisha wananchi wa vijijini kuendelea na adha ya maji huku akieleza kuwa miradi hiyo ilikuwa ikijengwa kwa gharama kubwa ikilinganishwa na uhalisia wa soko.

Mhandisi huyo pia amesema pamoja na utekelezaji wa mpango wa bajeti 2021/2022, kuliibuka pia uhitaji wa mradi wa maji kwa wananchi wa Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni ambacho wananchi kutoka Ngorongoro walihamia kwa hiari.

Katika kuboresho huduma ya maji Msomera, Serikali kupitia RUWASA inaendelea na ujenzi wa bwawa la maji kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.99 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 15. Ujenzi wa bwawa hilo utakapokamilika, utasaidia kuboresha huduma ya maji kwa wananchi na mifugo yao pia.

Kwa sasa, kati ya vijiji vyote nchini 12,319 ni vijiji 8,769 vinavyofikiwa na huduma ya uhakika ya maji safi na salama. Kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika mwezi Aprili, 2022 upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ulikuwa umefikia kiwango cha asilimia 74.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.7 ikilinganishwa na wastani wa 64.8 mwaka 2019. 

Amesema Kasi hii, ni nzuri na tukienda kwa kasi hii, tunatarajia kuvuka lengo la asilimia 85 ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. 

Kutokana na hayo ameeleza kuwa RUWASA inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji hicho, ambapo mpango wa utekelezaji uligawanywa katika awamu mbili (awamu ya muda mfupi na awamu ya muda mrefu).

Awamu ya muda mfupi imekamilika na vituo vya kuchotea maji 12 vimeshaanza kutoa huduma ya maji, awamu ya pili imefikia asilimia 70 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2022, kukamilika kwa awamu hiyo kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 17,000 pamoja na mifugo yao 

Hali hiyo itapelekea idadi ya vituo vya maji kuongezeka kutoka 12 hadi kufikia vituo vya kuchotea maji 30 kwa matumizi ya binadamu na vituo 3 vya kunyweshea maji mifugo

 Sambamba na hayo ameweka wazi kuwa Wakala huo unafanya jitihada kuboresha huduma ya maji katika Kijiji cha Msomera na kwamba Serikali kupitia RUWASA inaendelea na ujenzi wa bwawa la maji kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.99 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 15.

 Ujenzi wa bwawa hilo utakapokamilika, utasaidia kuboresha huduma ya maji kwa wananchi na mifugo yao

 

Post a Comment

0 Comments