CHONGOLO ATOA WITO KWA JUMUIYA YA WAZAZI KUWAJENGEA UWEZO VIONGOZI WA SHULE ZINAZOMILIKIWA NA CCM.


📌RHODA SIMBA

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ametoa wito kwa jumuiya ya wazazi wa Chama hicho  kuendelea kuwajengea uwezo viongozi wa shule ili heshima ya wakuu wa shule iendane na muda aliokaa katika shule.

Kadhalika amesema mpango wa chama hicho ni kuongeza tija katika kujenga mafanikio kwenye shule zinazomilikiwa na chama hicho.

Chongolo ameyasema hayo leo Juni 15,2022 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa semina ya watumishi wa taasisi za elimu zinazomilikiwa na jumuiya ya wazazi ya chama hicho.

Aidha amesema lengo la chama kuanzisha shule ni kuwawezesha vijana wote kupata elimu iliyobora ambapo katika matokeo ya mtihani mwaka huu karibu asilimia 80 hadi 90 ya wanafunzi wanaosoma katika shule zinazomilikiwa na chama wamepata ufaulu wa daraja la kwanza na la pili huku mwanafunzi mmoja tu akipata ufaulu wa daraja la nne.

Amesisitiza kwa wakuu wa shule kuendelea kujenga nidhamu katika shule wanazoziongoza katika kuendelea kujenga heshima ya chama.

Sambamba na hayo amebainisha kuwa heshima ya mwalimu ni matokeo bora hivyo amesisitiza kuwa awamu ijayo watatoa zawadi kulingana na kiwango cha ufaulu katika shule husika na kuwataka walimu kukaza buti katika ufundishaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Edmund Mndolwa amewataka watumishi katika taasisi za elimu zinazomilikiwa na chama kuacha kujihusisha na masuala ya siasa bali kujikita zaidi ufanikishaji wa utoaji wa elimu Bora.

Hata hivyo amesema kiwango cha ufaulu katika shule zinazomilikiwa na Chama zimeendelea kuimarika siku hadi siku kwani hakuna shule yoyote iliyopata daraja sifuri.

 

Post a Comment

0 Comments