JUMLA YA WAGONJWA 7113 WAFANYIWA UPASUAJI WA KIBINGWA

 

📌JASMINE SHAMWEPU

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Tib ana Mifupa Muhimbili (MOI) Dr Respicius Boniface ameelza kuwa Jumla ya wagonjwa 7,113 walifanyiwa upasuaji mbalimbali wa kibingwa hapa nchini ikilinganishwa na wagonjwa 6,793 waliofanyiwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wa 2020/2021 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 2%.

Hayo ameyasema leo Jijini Dododma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa upasuaji mbalimbali wa kibingwa uliofanyika ni pamoja na kubadilisha nyonga 207, kubadilisha magoti 168, upasuaji wa mfupa wa kiuno 96.  

"Wagonjwa 200 wamefanyiwa upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu na kati yao waliofanyiwa mabega ni 32 na magoti ni 168”

Dr Boniface ameeleza kuwa wagonjwa 249 wamefanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo kwa kufungua eneo dogo, watoto 17 wamefanyiwa upasuaji wa kunyoosha vibiongo na wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo.

Amefafanua kuwa gharama za matibabu hayo ndani ya nchi zilikuwa shilingi bilioni 10.2 na kama wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu, jumla ya Shilingi bilioni 42.7 zingetumika, hivyo taasisi imeokoa Shilingi bilioni 32.5 ambazo zitatumika kwa shughuli nyingine za maendeleo ya nchi 

Dr Boniface.

Aidha amezungumzia huduma mpya zilizoanzishwa MOI katika kipindi hiki kuwa ni pamoja na huduma ya kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua ambapo wagonjwa 19 wameshafanyiwa upasuaji. 

Katika hatua nyingine jumla ya wagonjwa 186 wamehudumiwa katika maabara ya upasuaji wa ubongo ambapo gharama za huduma hii hapa nchini ni kati ya Shilingi milioni 5-10 na nje ya nchi ni Shilingi milioni 30 mpaka 60, hivyo Taasisi imeokoa kati ya Shilingi bilioni 5.6 hadi Shilingi bilioni 11.2 ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa hao nje ya nchi.

Ili kufikia mafanikio hayo makubwa, Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) imetoa pongezi kwa Serikali ambapo imetenga Shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya ununuzi wa mashine mpya ya kisasa ya MRI na CT scan pamoja na vifaa vya chumba cha tiba Mtandao vya Shilingi milioni 227 kwa ajili ya kuimarisha huduma hiyo nchini.

Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Taasisi ya MOI amekiri kuwa serikali ilitoa kiasi cha Shilingi bilioni 4.2 kwa ajili ya ununuzi wa vipandikizi ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vipandikizi hivyo kwa wagonjwa.

Vifaa hivi vimesaidia kuendelea kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa ya mifupa, ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi na fedha za Serikali ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu na kuongeza kwa huduma hiyo mpya imeiwezesha taasisi kupunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa nje ya nchi

Kwa sasa kwa magonjwa ya 'Neurosurgeries' kwa asilimia 96 tunafanya hapa pamoja na asilimia 98 ya upasuaji wa mifupa tunafanya hapa nchini," aliwaambia waandishi wa habari.

Kuhusu huduma za karakana ya viungo bandia, amesema zimeendelea kuimarika, katika kipindi hiki ambapo jumla ya viungo bandia 411 vimetengenezwa na Wakati huo huo, Taasisi imeanzisha huduma mpya ya utengenezaji wa mkono wa umeme ambapo tayari wagonjwa watatu wameshahudumiwa, ambapo gharama zake ndani ya nchi ni Shilingi milioni 15 na nje ya nchi ni Shilingi milioni 30 mpaka 60

Vile vile Taasisi ya MOI imeingia mkataba na Hospitali ya Nyangao Lindi na Ndanda Mtwara kwa lengo la kusogeza huduma kwa Wananchi wa Mikoa ya Kusini ambapo katika kipindi hiki wagonjwa 3,441 walihudumiwa katika kliniki za kawaida na kuwafanyia upasuaji wagonjwa 731.

Uanzishwaji wa huduma mpya ya kliniki jongefu; zaidi ya wagonjwa 510 wameshahudumiwa katika Wilaya ya Temeke na upasuaji kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi katika hospitali ya Hydom Arusha ambapo wagonjwa 60 walifanyiwa upasuaji huo," alieleza Mkurugenzi huyo Mtendaji wa MOI.

Kwa upande wa Mafunzo na kuimarisha utendaji kazi Taasisi hiyo imeshiriki kwenye kujengea uwezo Wataalamu wa hospitali kubwa za Bugando, Mbeya, KCMC na Benjamin Mkapa na kuendelea kuwa na ushirikiano mzuri na Taasisi za kimataifa za nje katika kufanya kambi za upasuaji wa wagonjwa, mafunzo kwa wataalamu wetu, Tafiti na misaada ya vifaa Tiba

Katika kipindi hiki, taasisi imeingia mkataba wa ushirikiano na Chama cha madaktari cha nchini China (CMA) na Hospitali ya Tian Tan ya Beijing China Peking – Katika kuendeleza fani ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.

Tumeingia Mkataba pia na hospitali ya Ramaiah ya Bangalore India – katika kuendeleza fani ya upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu kichwani pasipo kufungua fuvu la kichwa na kuongeza kuwa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha MUHAS, imeendelea kufundisha wataalamu (mabingwa) wa mifupa, mishipa ya fahamu na upasuaji wa ubongo na imeendelea kuwa hospitali ya kufundishia ya Chuo Cha ubingwa wa upasuaji katika nchi za Afrika ya Mashariki, Afrika Kusini na Afrika ya Kati (COSECSA).

Taasisi ina mpango wa kuendelea kuboresha huduma zetu, kujenga hospitali ya kisasa ya utengamano (Rehabilitation centre) katika kiwanja cha MOI chenye ukubwa wa hekari 10 kilichopo Mbweni Mpiji jijini Dar es salaam pamoja na kuendelea kusogeza huduma zetu kwa wananchi.

Pamoja na pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuongoza nchi ikiwemo kuboresha huduma za Afya hapa nchini, Taasisi ya MOI ina jukumu la kutoa tiba za kibingwa kwa magonjwa ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu, kufundisha na kuongeza wataalamu wa fani hizi nchini pamoja na kufanya tafiti za magonjwa hayo ili kuboresha tiba.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, huduma katika taasisi ya MOI zimeendelea kuboreshwa na kuimarika ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kisasa, zikiwemo; ICU Ventilators, Monitors, vitanda na Ambulance ya kisasa (Vyenye thamani ya Shilingu billion 1.3 zilizotolewa na Serikali).

 

Post a Comment

0 Comments