RAIS SAMIA AAGIZA MNARA WA MASHUJAA UJENGWE KWA KIWANGO CHA HADHI YA MAKAO MAKUU DODOMA

 

📌RHODA SIMBA 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuja na mpango wa kujenga mnara wa mashujaa katika makao makuu ya nchi wenye hadhi ya makao makuu.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Julai,25,2022 jijini Dodoma katika maadhimisho ya siku ya mashujaa kitaifa

“Kwa kuwa jiji la Dodoma linakua, nipendekeze Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutafuta eneo kubwa na bora zaidi kujenga mnara wenye hadhi ya makao makuu ya nchi kwa gharama zitakazostahimilika au kwa gharama nafuu vilevile nipendekeze kuja na mpango wa kuwa na maadhimisho yenye gharama nafuu zaidi”amesema.

Aidha,Rais samia amesema mashujaa wanamchango mkubwa hali ambayo imesababisha Tanzania kujijengea heshima kwa mataifa kwa kuendelea kudumisha amani.

Kuhusu suala la uamuzi wa serikali kuhamia makao makuu Dodoma Rais Samia amesema mpango upo palepale.

“Naomba nirudie kauli ya Hayati Magufuli kuwa mpango wa Serikali ya kuhamia makao makuu Dodoma upo palepale hakuna kurudi nyuma” amesisitiza.

Ikumbukwe kuwa siku ya Maadhimisho ya Mashujaa hufanyika Julai 25 kila mwaka kama ishara ya kuwakumbuka mashujaa wa taifa waliopoteza maisha kwa kulipigania taifa lao na kulinda uhuru na hufanyika shughuli mbalimbali ikiwemo dua na sala maalum na gwaride maalum ambapo mwaka huu kitaifa yamefanyika jijini Dodoma na mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Samia Suluhu Hassan akiambatana na viongozi wakuu mbalimbali wa Serikali.



 

 

Post a Comment

0 Comments