JAMII YAASWA KUWAJALI NA KUWAWEZESHA WATU WENYE ULEMAVU


Fundi Mkuu wa Karakana ya watu wenye ulemavu Dodoma, Mwita Marwa akiwa katika shughuli zake za utengenezaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu


📌SALMA HAROUN & JOSEPHINE MTWEVE

JAMII imetakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwajali na kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii kwa lengo la kujenga umoja na kuwafanya wajihisi wana nafasi ya kushiriki vitu mbalimbali kama watu wengine.

Mwita Marwa ambaye ni mlemavu wa miguu lakini pia ni fundi mkuu katika Karakana ya watu wenye ulemavu Dodoma (KAWADO) inayohusika na utengenezaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ameishauri jamii iwakumbuke na kuwajali watu hao.

Marwa ameiomba serikali kwa kushirikiana na Taasisi na Makampuni iwawezeshe watu wenye ulemavu kwa kuwapa mitaji na kuendeleza vipaji vyao kwa kuwasomesha vyuo vinavyohusika na fani mbalimbali ili kuwaepusha na suala la utegemezi kwa watu wengine.

Mimi hapa natengeneza vifaa vya kuwasaidia walemavu lakini pia sijaajiri watu ila nina vijana ninaosaidiana nao kazi lakini pia nafundisha watu wengine wenye ulemavu kama mimi ambao wengine mpaka sasa tayari wamefungua ofisi zao sehemu nyingine na zinawasaidia kuendesha maisha yao

Marwa.

Aidha Marwa amewataka walemavu kubadilika na kuhakikisha wanajikita katika shughuli za kijamii kama biashara kwa kuomba mitaji kwa watu wenye uwezo katika jamii kwa lengo la kuepuka utegemezi kwa watu wengine.

"Mimi sikusomeshwa na wazazi wangu ila nilijisomesha mwenyewe elimu ya shule ya msingi lakini nikapata msaada wa kwenda chuo cha ufundi na mpaka sasa mimi ndo msaada kwa wazazi wangu na kwa watu wengine wenye ulemavu

 Marwa.

Kwa upande wake mmoja wa wafanyakazi katika karakana hiyo Michael amesema kutokana na upeo mdogo wa watu wanaona watu wenye ulemavu hawana msaada katika jamii lakini Marwa ni moja kati ya walemavu waliothubutu kuonyesha uwezo wake katika jamii.

Amesema jamii inatakiwa kuwachukulia watu wenye ulemavu kuwa kama watu wengine ambao wanauwezo wa kufanya kazi kutokana na wote kuwa na haki sawa katika kujumuika na kushiriki mambo mbalimbali ya kijamii.

 

 

Post a Comment

0 Comments