MHE JENISTA ARIDHISHWA NA NAMNA e-GA INAVYOWEZESHA VIJANA WA VYUO VIKUU KUFANYA TAFITI NA UBUNIFU WA MIFUMO YA TEHAMA KATIKA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOKABILI SEKTA MBALIMBALI NCHINI

 

📌VERONICA MWAFISI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameridhishwa na kazi inayofanywa na vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), mifumo ambayo itasaidia kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo katika sekta ya kilimo, nishati, madini na uchumi.

Mhe. Jenista amesema hayo, mara baada ya kukitembelea Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na kujionea kazi inayofanywa na vijana hao wa vyuo vikuu waliochukuliwa na e-GA kwa lengo la kuwajengea uwezo katika eneo la utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA ambayo itakuwa na tija katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, kuna utafiti mkubwa wa kimkakati unaofanya na vijana hao wa vyuo vikuu, ambao utaiwezesha Serikali kukusanya mapato ya kutosha yatakayotumika na Serikali katika kuleta ustawi wa taifa na maendeleo ya wananchi.

Ninaipongeza menejimenti ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kuwa na mkataba maalum unaowawezesha kuwapata hawa vijana kutoka vyuo vikuu ili kuwapatia mafunzo kwa njia ya vitendo kwenye eneo la utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA itakayolisaidia taifa kuingia kwenye uchumi wa kidigitali

Mhe. Jenista 

Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, matokeo ya kazi nzuri ya utafiti na ubunifu huo wa mifumo ya TEHAMA, yatakuwa ni utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwani mifumo hiyo itawarahisishia wananchi kupata huduma bora na kwa wakati katika taasisi za umma.

Kupitia mifumo itakayobuniwa, huduma zitatolewa kwa wananchi kwa gharama nafuu, mapambano dhidi ya rushwa yataimarika, mapato ya serikali yataongezeka ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa usimamizi wa matumizi sahihi wa fedha za umma

Mhe. Jenista 

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema kuwa, utafiti na ubunifu unaofanywa na vijana wa Vyuo Vikuu kupitia Kituo hicho unaonesha kuwa taifa limeanza kupiga hatua kwa kuwatumia vijana kuleta maendeleo, na kuongeza kuwa alichojifunza ni kuwa, kama nchi tunaweza kuwatumia vijana katika tafiti na bunifu zenye tija kwa taifa.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) amesema kwa sasa Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha e-GA kina uwezo wa kuchukua wanafunzi wa mazoezi kwa njia ya vitendo wapatao 100, lakini mamlaka ina mpango wa kuongeza uwezo wa kituo ili hapo baadae kiweze kuchukua wanafunzi kati ya 300 hadi 500 kwa wakati mmoja.

Mmoja wa vijana walionufaika na kituo hicho, Bw. Edward Sultan amesema Serikali kwa upande wake imeshatekeleza wajibu wake wa kuanzisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha e-GA ambacho kina vitendea kazi vyote vinavyohitajika, hivyo ni jukumu la vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti, ubunifu waliopata nafasi ya kufanya mazoezi kwa njia ya vitendo kufikiri walifanyie nini taifa ambalo limewapa fursa ya kutoa mchango katika eneo la utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA.

Mnufaika mwingine wa kituo hicho, Bi. Lina Lajo ameshukuru kupata fursa ya kujifunza kwa njia ya vitendo katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha e-GA na kuongeza kuwa, kituo hicho ni sehemu nzuri ya kujifunza na kutoa mchango kwa taifa kama vijana.

Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kilianza kupokea wanafunzi wa mazoezi kwa njia vitendo kutoka katika vyuo vikuu kuanzia mwaka 2019 mpaka sasa 2022 ambao wameshiriki katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA kama vile Mfumo wa e-Mrejesho, Mfumo wa e-Mikutano, Mfumo wa e-Dodoso na Mfumo wa e-Board ambayo inatumika hivi sasa Serikalini.





 

 

Post a Comment

0 Comments