TANNA YAIOMBA SERIKALI KUPITIA UPYA MUUNDO MPYA WA UTAWALA WA SERIKALI ZA MITAA

 

📌JOSEPHINE MTWEVE

SERIKALI imeombwa kupitia upya muundo mpya wa utawala wa Mamlaka za Serikali za mitaa Tanzania wa mwaka 2022 ambao umetajwa kutotendea haki upande wa uuguzi na ukunga kwa lengo la kuboresha na kutoa huduma zilizobora kwa uangalizi stahiki.

Hayo yamesemwa na Alexander Mauliya ambae ni Raisi wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA) ambacho ni Cha kitaaluma kinachotetea na kushirikiana na Serikali kushawishi kutengeneza mazingira rafiki kwa wanataaluma amesema baada ya kupitia muongozo huo na kushauriana na wadau mbalimbali waliona haujatendea haki taaluma ya uuguzi na ukunga.

Amesema changamoto za afya zipo nyingi lakini huenda zinaweza kuongezeka endapo muundo huo utaendelea kutekelezwa na utatoa fursa ya kukosa usimamizi bora wa kazi kwa ukaribu kutokana na kutotambulika katika ngazi za halmashauri.

Mfano unaposhindwa kutambua muongozo wa Wauguzi katika halmashauri za mikoa nani atakayesimamia ambae atakuwa anajua changamoto iliyotokea ya kitaaluma? sasa leo unapoondoa Mamlaka za kiutawala kwenye halmashauri zetu za uuguzi na ukunga tafsiri yake unaenda kudhoofisha huduma ambazo sisi tumeziona za muhimu sana

Amesema idara iliyokuwepo mwanzoni ilikuwa ikisimamiwa na mganga mkuu wa Wilaya ambae alikuwa akisimamia kada zote zilizo chini yake zinazohusika na masuala ya afya lakini kutokana na maboresho ya muundo huo mpya huduma ya uuguzi na ukunga haijatambulika.

Aidha ameiomba Serikali kusitisha muundo huo na kufanyia kazi mapendekezo yao ambayo yaliwasilishwa mwezi Mei 31 mwaka huu baada ya kilele cha maadhimisho ya uuguzi na ukunga duniani ambapo waliahidiwa kufanyia kazi.

Hatukuishia hapo tuliwaandikia Wizara husika mapendekezo yetu lakini mpaka muda huu hatujapata mrejesho na tulifanya jitihada za kuuona uongozi wa Wizara hatujafanikiwa

Hata hivyo amesema chama kiko tayari kuitwa kukaa pamoja na Wizara husika kujadili na kushauriana ili maboresho yawe shirikishi, Ili wanapoenda kujipanga kuhudumia jamii kila mtu awe anajua wajibu wake na stahiki zake na nini kifanyike hatimaye waweze kutoa huduma zilizo bora.

Post a Comment

0 Comments