TRC LIMEJIPANGA KUBORESHA MIUNDO MBINU ILI KURAHISISHA SHUGHULI ZA KIUCHUMI.

 


📌RHODA SIMBA

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limesema limejipanga kutekeleza mipango ya kitaifa katika uboreshaji na uendelezaji wa miundombinu ili kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kukuza biashara ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa shirika hilo Masanja Kadogosa wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya shirika la (TRC) kwa mwaka 2021/22.

Aidha amesema kuwa pamoja na kuwa na majukumu mengine pia shirika hilo kwa mwaka wa fedha 2021/22-2022/23 limejikita zaidi katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa shirika kwa kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu ya Reli ununuzi na ukarabati wa vitendea kazi.

Ili kufikia adhma ya ufanisi, shirika litahakikisha linaboresha miundombinu ya Reli kwa kujenga mtandao mpya wa Reli wa kiwango cha Standard Gauge wenye jumla ya kilometa 4,777 na ukarabati mtandao wa Reli iliyopo ya Meter Gauge kwa kilometa 2537

Amesema, ukarabati huo wa njia utajumuisha kuinua uwezo wa njia kwa kuondoa reli nyepesi za paundi 45 na 56 na kutandika Reli nzito za paundi 80, kuinua uwezo wa madaraja kutoka ekseli 13.5 kufikia ekseli 18.5 pamoja na kuboreshwa mfumo wa ishara na mawasiliano.

Amesema upande wa miradi shirika linatekeleza miradi ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu. Muda mfupi inajumuisha miradi ya ufufuaji wa njia za zamani ikiwemo njia ya kaskazini ,miradi ya muda wa kati inajumuisha ukarabati wa njia iliyopo ikiwemo uboreshaji wa njia ya kati ambao umefanyika kupitia Mradi wa Tanzania Intermodal and Tall Development project (TIRP) kutoka Dar es salaam hadi Isaka, Miradi ya muda mrefu ni pamoja na Mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR).

Serikali inajenga mfumo wa umeme wa msongo wa kilovoti 220 ambao unajitegemea (dedicated line) kwa ajili ya uendeshaji wa treni ili kupata umeme wa uhakika, Kwa kipande Cha Dar es salaam mpaka Morogoro mfumo huo una urefu wa kilimeta 160 na umekamilika kwa asilimia100, mkandarasi ameshalipwa kiasi cha bilioni 70.6

 Mkurugenzi huyo pia amefafanua kuwa, kipande cha Morogoro mpaka Makutupora ujenzi wa msongo wa kilovoti 220 ambao unaendelea una jumla ya kilimeta 410 na mkataba wake ni shilingi bilioni 160.2

Kwa upande wake Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema ujenzi wa reli hiyo unaenda sambamba na maboresho ya bandari zilizopo nchini kwa kuwa miundombinu hiyo ni mahsusi kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo mizito.

 

Post a Comment

0 Comments