WIZARA, WADAU KUTATUA TATIZO LA WATOTO MITAANI

 ðŸ“ŒWMJJWM

SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha inapunguza tatizo la Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Akizungumza katika kikao na Taasisi ya Azaria Foundation Jijini Dodoma Agosti 22, 2022 Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula ameitaka jamii kuwa na upendo kati ya familia na kuhakikisha watoto wanatunzwa katika familia ili wapate Malezi na Makuzi bora katika ukuaji wao.

Dkt. Chaula amesema pamoja na kuwa mwanzilishi wa Taasisi hiyo ni zao la watoto walioishi mazingira magumu baada ya kutelekezwa na familia yake amekuwa msaada kwa watoto wengine ili wasiendelee kuishi maisha hayo.

Familia inaposhindwa kwa namna yoyote ile, sisi Jamii tuchukue wajibu na tuungane na Wadau hawa kutatua shida hii, Wizara tumejipanga kwa kushirikiana na Wadau kutumia mbinu zote

Dkt Chaula

Naye Mkurugenzi na mwanzilishi wa Taasisi ya Azaria Foundation, Audax Abeli ambaye ameishi maisha ya mtaani amesema familia yake ilikuwa chanzo cha yeye kuitwa Mtoto wa mtaani jina ambalo siyo sahihi hivyo namna bora ya kuwatoa watoto hao mtaani ni kuanzia upendo kwao.

Hili tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani linatakiwa kushughulikiwa kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa, tunaweza tukapunguza watoto wa mtaani. Pia changamoto nyingine zinatokana na familia

 Audax.

Ameeleza kuwa mpaka sasa Taasisi hiyo inahudumia jumla ya watoto 70 kwa kuwapatia huduma muhimu za kijamii na kuwapatia mbinu mbadala za kupambana na maisha.

Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera Mhando amesema Wizara itashirikiana vyema na mdau wa Taasisi hiyo kwa kusaidiana na timu ya wataalamu inayofanya kazi ya kushughulikia watoto wanaoishi mazingira magumu na kuwatoa mtaani.

Mojawapo ya mradi utakaozinduliwa hivi karibuni ni mradi wa ujenzi wa kituo cha kupokea watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na kuwapitisha katika mabadiliko ya tabia na ujuzi ili wanaporudi majumbani waweze kujiajiri

Dkt. Nandera.


Post a Comment

0 Comments